2014-12-01 10:03:06

Papa "achonga" na waandishi wa habari wakati akirejea mjini Vatican


Baba Mtakatifu Francisko wakati akirejea mjini Vatican kutoka Uturuki, Jumapili alasiri, 30 Novemba 2014, amepata nafasi ya kuzungumza na waandishi wa habari kwa dakika 45 katika safari ya masaa matatu na robo. Mambo makuu yaliyojitokeza katika mazungumzo haya ni: umuhimu wa majadiliano ya kidini kati ya Wakristo na Waislam.

Baba Mtakatifu amekazia umuhimu kwa watu kuendelea kusali ili kuombea haki, amani, upatanisho na ustawi miongoni mwa watu; umuhimu wa Makanisa kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kiekumene, ili kufikia umoja kamili; ukweli na uwazi katika maisha na utume wa Kanisa; umuhimu wa Sinodi; tatizo la wakimbizi na madhara yanayotokana na biashara haramu ya silaha inayoendelea kusababisha majanga makubwa duniani.

Wakristo na Waislam hawana budi kushikamana katika kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini, ili kujenga na kuimarisha misingi ya haki, amani na utulivu kati ya watu kwa kuondokana na vitendo vya kigaidi ambavyo vimekuwa ni chanzo kikuu cha maafa kwa watu na mali zao. Waamini wakuze na kujenga misingi ya amani kwani ndilo chimbuko la kila dini.

Amani ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inapaswa kuwawajibisha viongozi wote wa kisiasa, kidini, kijamii na kitamaduni kwa kupinga na kulaani vitendo vyote vya kigaidi, ili watu waweze kuishi kwa amani na utulivu kwa ajili ya ustawi na maendeleo yao kiroho na kimwili. Tofauti za kidini zisiwe ni chanzo cha vita na kinzani za kijamii.

Baba Mtakatifu anasema, amekwenda nchini Uturuki kama mhujaji na wala si mtalii, ili kushiriki pamoja na Patriaki Bartolomeo wa kwanza maadhimisho ya Siku kuu ya Mtakatifu Andrea. Alipotembelea Msikiti mkuu wa Bluu ulioko Istanbul, Baba Mtakatifu anasema, amesikiliza kwa umakini mkubwa simulizi la kuzaliwa kwa Yohane Mbatizaji. Amesali kwa ajili ya kuombea amani nchini Uturuki pamoja na kuombea amani, sehemu mbali mbali za dunia ambazo kwa sasa zimetumbukia katika vita.

Baba Mtakatifu anasema, majadiliano ya kiekumene yanaendelea kati ya Kanisa Katoliki na Patriaki wa Moscow na kwamba, katika miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na mahusiano mazuri, kiasi hata cha ujumbe kutoka kwa Patriaki wa Kanisa la Kiorthodox la Moscow umeshiriki katika maadhimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu kuhusu Familia. Kuna majadiliano ya kitaalimungu yanayoendelea kati ya Makanisa haya mawili, lakini ikumbukwe kwamba, umoja wa Kanisa ni hija ndefu inayoyashirikisha Makanisa yote katika maisha ya kiroho; matendo ya huruma na ushuhuda wa pamoja kiasi hata cha Wakristo kuyamimina maisha yao kama walivyofanya Mashahidi wa Uganda, waliotangazwa kuwa Watakatifu miaka 50 iliyopita.

Majadiliano ya kiekumene hayana budi kujichimbia katika uhalisia wa maisha ya Wakristo kwa kushirikishana rasilimali na utajiri uliopo, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo. Patriaki Kirill ameonesha utayari wa kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko, lakini kwa sasa kinachokwamisha ni vita na kinzani zilizoko huko Ucrain.

Katika majadiliano ya kiekumene anasema Baba Mtakatifu, Kanisa Katoliki litaendelea kuhamasisha umoja kamili kati ya Wakristo bila kulazimishana, bali kumwachia Roho Mtakatifu ili aweze kuliongoza Kanisa la Kristo, bila kujiangalia wala kujitafuta lenyewe. Kanisa ni takatifu kwa vile limeanzishwa na Yesu, lina dhambi na mapungufu yake kwani linaongozwa na binadamu, changamoto kwa Makanisa kuangalia maisha na utume wa Kanisa la mwanzo, ili kusonga mbele kwa imani na matumaini makubwa.

Baba Mtakatifu anasema bado kuna changamoto nyingi zinazopaswa kufanyiwa kazi kwa mfano kuwa na tarehe moja ya Maadhimisho ya Siku kuu ya Pasaka. Hapa kuna haja ya kuendeleza majadiliano katika ukweli na uwazi; Katekesi ya kina pamoja na kuheshimiana, kwani majadiliano ya kweli yanajengeka katika ukweli, uvumilivu na busara.

Baba Mtakatifu anasema, maadhimisho ya Sinodi ni hija ndefu inayohitaji nafasi ili kufanya tafakari ya kina, kwa kumwachia Roho Mtakatifu kuliongoza Kanisa. Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Familia iliyohitimishwa tarehe 19 Oktoba 2014 walifuata mchakato mzima wa maadhimisho ya Sinodi na hatimaye, wakatoa hati ya Mababa wa Sinodi, ambayo itatumika kama Mwongozo wa kazi utakaotumwa kwa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali duniani. Waamini wajitahidi kutoa nafasi kwa Roho Mtakatifu kutenda kazi yake ndani ya Kanisa.

Baba Mtakatifu bado anaendelea kuonesha utashi wake wa kuwatembelea wananchi wa Iraq ili kushiriki pamoja nao shida na mahangaiko, lakini ukweli wa mambo ni kwamba, jambo hili kwa sasa haliwezekani, ndiyo maana wakati wa hija yake ya kiekumene amebahatika kukutana na kuzungumza na vijana wakimbizi kutoka Iraq wanaohudumiwa na Wasalesiani wa Don Bosco. Takwimu zinaonesha kwamba, kuna wakimbizi millioni moja ambao wanahitaji msaada wa dharura; usalama ni kikwazo kikubwa!

Baba Mtakatifu kwa mawazo yake binafasi anasema, chuki na uhasama, migogoro ya kivita na kinzani za kisiasa na kijamii; athari za myumbo wa uchumi kimataifa; majanga asilia pamoja na biashara haramu ya silaha duniani, ni kati ya mambo yanayotoa kipaumbele cha kwanza kwa fedha na kumweka Mungu pembezoni wa mipango na mikakati ya binadamu. Vita kuu ya kwanza na ya pili ya Dunia bado havijatoa fundisho la kutosha kwa binadamu, ndiyo maana binadamu anaendelea kutengeza silaha za mahangamizi dhidi ya binadamu na hivyo kuchangia kuharibu mazingira. Zote hizi ni dalili za kuzuka kwa Vita kuu ya Tatu ya Dunia.

Baba Mtakatifu Francisko anatamani kuona mpaka kati ya Uturuki na Armenia ukifunguliwa kama kielelezo cha mwanzo wa mchakato wa upatanisho kati ya mataifa haya mawili. Kuna matukio makubwa yanayotarajiwa kuadhimishwa kwa ajili ya kufanya kumbu kumbu ya kinzani zilizojitokeza baina ya mataifa haya mawili. Baba Mtakatifu Francisko mwishoni, amewataka wanahabari kuendelea kuwahabarisha walimwengu yale yanayotendeka, bila kusahau kusali kwa ajili ya maisha na utume wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa. C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio VaticanAll the contents on this site are copyrighted ©.