Hija ya kiekumene ya Papa Francisko nchini Uturuki ilisheheni utajiri mkubwa wa maisha
ya kiroho na kiutu!
Padre Federico Lombardi Msemaji mkuu wa Vatican akifanya rejea ya hija ya kiekumene
ya Baba Mtakatifu Francisko aliyoihitimisha, Jumapili alasiri anasema kwamba, Baba
Mtakatifu aliianza siku yake ya mwisho kwa kukutana na kuzungumza na Bwana Isak Haleva,
Rabi mkuu wa Uturuki na baadaye alishiriki kwenye Ibada ya Liturujia Takatifu iliyoongozwa
na Patriaki Bartolomeo wa kwanza, kama sehemu ya Maadhimisho ya Siku kuu ya Mtakatifu
Andrea, msimamizi wa Kanisa la Costantinopoli.
Ibada hii ilisheheni utajiri
mkubwa wa Neno la Mungu uliosindikizwa kwa nyimbo. Neno la Mungu lililosomwa katika
Ibada hii ni sehemu ya Injili inayoonesha wito wa Andrea Mtume aliyekutana kwa mara
ya kwanza na Yesu, baadaye akamwahabarisha ndugu yake Simoni na tangu wakati huo,
wote wawili wakaacha yote na kuanza kuandamana na Yesu katika maisha na utume wake.
Hii imekuwa ni Injili ya Makutano kati ya Yesu na Wafuasi wake, tukio ambalo
limeendelezwa na Patriaki Bartolomeo wa kwanza pamoja na Baba Mtakatifu Francisko,
ambao kwa pamoja wamekazia umuhimu wa Wakristo kukutana na kutembea kwa pamoja kama
ndugu katika Kristo, kama ilivyokuwa kwa Mitume wa Yesu walipokutana na Yesu, wakamwona
na kubaki daima pamoja naye katika maisha yao yote.
Liturujia Takatifu ilikuwa
na utajiri pamoja na mvuto mkubwa kwa waamini, jambo ambalo limetiliwa mkazo pia na
Baba Mtakatifu Francisko kwa kusema kwamba, utajiri wa Neno la Mungu kutoka katika
Makanisa mbali mbali ni muhimu sana kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa ndiyo
maana Baba Mtakatifu Francisko aliamua kushiriki katika Ibada hii, ili kuonesha utashi
wa kiekumene wa kutaka kujenga na kudumisha umoja miongoni mwa Wakristo, siyo tu wakati
wa kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu.
Kipaumbele cha kwanza ni kukaa
kwa pamoja, ili hatimaye, kuamsha nia ya kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa kwa pamoja.
Baba Mtakatifu ameshiriki Ibada hii kwa moyo wa uchaji na heshima kubwa, kwani Liturujia
Takatifu ni sehemu muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa la Kiorthodox, ndiyo
maana, Mapapa wanapotembelea Kanisa la Kiorthodox wanapenda kushiriki katika Liturujia
Takatifu, inayoonesha umoja na utofauti hata katika lugha, kama ilivyo hata katika
Kanisa Katoliki.
Padre Lombardi anasema kwamba, hotuba zilizotolewa na viongozi
hawa wawili zilikuwa na umuhimu wa pekee katika mchakato wa kuendeleza majadiliano
ya kiekumene, ili hatimaye, kuweza kufikia umoja kamili miongoni mwa Wakristo. Patriaki
Bartolomeo wa kwanza anasema, lengo si kusafisha na kuponya madonda ya utengano yaliyojitokeza
katika historia, bali kuangalia mbele kwa imani na matumaini kwani Kanisa Katoliki
na Papa wanayo nafasi muhimu sana katika majadiliano ya kiekumene. Khalifa wa Mtakatifu
Petro anaonesha ukuu pamoja na dhamana ya upendo na huduma mintarafu mwelekeo wa Kisinodi;
mambo msingi katika hija ya kuelekea katika umoja kamili kati ya Wakristo.
Baba
Mtakatifu Francisko katika hotuba yake amekazia kwamba, umoja wa Kanisa haulengi kutweza
au kuyameza Makanisa, bali kushirikishana karama na utajiri unaofumbatwa katika Makanisa
haya, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo, kwani kielelezo cha madaraka
ya hali ya juu ndani ya Kanisa kinajionesha katika huduma ya upendo. Makanisa hayana
budi kuendelea kushirikiana na kushikamana katika kulinda na kutetea utu na heshima
ya binadamu; kuwasaidia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii; kudumisha
haki, amani na upatanisho kati ya watu; kulinda na kutunza mazingira pamoja na kuwasaidia
vijana kupambana kwa ushupavu na changamoto katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo
ya sayansi na teknolojia.
Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake amelaani
mauaji ya watu wasiokuwa na hatia yanayofanywa kwa kisingizio cha dini, kama inavyotokea
nchini Nigeria, changamoto kwa waamini wa dini mbali mbali kushikamana kwa pamoja
kupinga vitendo vya kigaidi vinavyoendelea kusababisha majanga makubwa katika maisha
ya watu sehemu mbali mbali za dunia.
Viongozi hawa wakuu wa Makanisa anasema
Padre Lombardi, wamekazia umuhimu wa kuendeleza na kudumisha mambo msingi yanayoyaunganisha
Makanisa na kwamba, maandalizi ya Mtaguso mkuu wa Makanisa ya Kiorthodox utakaofanyika
kunako mwaka 2016 ni hatua muhimu sana katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene,
kama Kanisa Katoliki lilivyofanya kwa Maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.
Hili ni tukio la matumaini kwa Makanisa yote.
Viongozi hawa wawili anasema
Padre Lombardi wametia sahihi kwenye Tamko la Pamoja na wala hawakusoma, kwani ni
mwendelezo wa hija iliyokwishafanywa na Makanisa haya, wakati wa hija ya kitume ya
Baba Mtakatifu Nchi Takatifu, mwezi Mei, 2014. Tamko hili limegusia vita na kinzani
za kidini zinazoendelea kujitokeza huko Mashariki ya Kati; umuhimu wa kujenga na kudumisha
majadiliano ya kidini na Waamini wa dini ya Kiislam pamoja na mchakato wa ujenzi wa
amani nchini Ucrain.
Hii ni kumbu kumbu ya maadhimisho ya Miaka 35 tangu Mtakatifu
Yohane Paulo II alipotia sahihi kwenye Tamko la Pamoja kuhusiana na Majadiliano ya
Kitaalimungu kati ya Makanisa haya mawili na Patriaki Dimitrios wa kwanza. Tume hii
imepewa dhamana ya kujadili na kutafuta ufumbuzi wa changamoto na matatizo yanayokwamisha
mchakato wa umoja kamili kati ya Makanisa.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican.