Watawa jikiteni katika Injili, Unabii na Matumaini!
Kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, Kardinali Joao Braz de Avis, Mwenyekiti wa
Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume, Jumapili tarehe 30 Novemba
2014 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuzindua Mwaka wa Watawa Duniani
utakaofikia kilele chake hapo tarehe 2 Februari 2016, kwa kuwataka watawa kujikita
zaidi na zaidi katika Injili; Utume na Unabii, huku wakijiaminisha chini ya ulinzi
na usimamizi wa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa.
Kardinali De Avis anasema,
Baba Mtakatifu Francisko alitamani kuwepo kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu
Petro hapa mjini Vatican kwa ajili ya kuzindua Mwaka wa Watawa, lakini kutokana na
uzito wa hija ya kiekumene, hakufanikiwa, lengo ni kuendeleza majadiliano ya kiekumene
na kidini kati ya waamini wa dini mbali mbali, ili kujenga na kudumisha mshikamano
wa dhati.
Nia ya Baba Mtakatifu katika Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa ni kuhakikisha
kwamba, watawa wanaendelea kujitosa bila ya kujibakiza kwa kuonesha upendo wao kwa
Mwenyezi Mungu, huku wakikumbatia Mashauri ya Kiinjili, ambayo ni: Ufukara, usafi
kamili na utii. Kanisa linauzindua Mwaka wa Watawa kwa kuonesha matumaini yake kwa
Mwenyezi Mungu ambaye daima amekuwa mwaminifu na mwingi wa huruma na mapendo; anayebatilisha
ukosefu wa uaminifu kwa njia ya huruma yake na kwamba, mtu anayemtumaini kamwe hataweza
kudanganyika.
Kardinali De Avis anasema, hata watawa wanapaswa kujisikia kutoka
katika undani wa maisha yao kwamba, wanahitaji kuonja huruma na upendo unaobubujika
kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kama ilivyokuwa kwa Waisraeli wanaosimuliwa katika Liturujia
ya Neno la Mungu, kwa kumwonesha Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, ili kuwa karibu
zaidi na binadamu na watawa wanayo kila sababu ya kusema, " Ee Bwana, wewe u baba
yetu; sisi tu udongo, nawe u mfinyanzi wetu, sisi sote tu kazi ya mikono yako." Na
Mwinjili Marko anawataka waamini kukesha na kusali; mambo msingi katika Maadhimisho
ya Mwaka wa Watawa Duniani.
Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake kwa
Watawa katika Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa inayojulikana kama "Mashahidi wa Furaha",
anawataka watawa kuwa kweli ni chemchemi ya furaha, wakionesha kwamba, Mwenyezi Mungu
anaweza kuwakirimia furaha ya kweli bila ya kuwa na kishawishi cha kutafuta furaha
hii mahali pengine popote.
Baba Mtakatifu anasubiri kwa hamu kuona watawa wakiwaamsha
walimwengu kwa njia ya Unabii, kwa kujikita katika Injili, changamoto kwa Familia
nzima ya Mungu, lakini watawa wanawajibika zaidi kwani wao wamechagua kuacha yote
kwa ajili ya Mungu na jirani. Watawa wawe ni mashahidi wanaoshuhudia maisha ya Yesu
hapa duniani na kwamba, hiki ni kipaumbele cha pekee kwa watawa.
Watawa wanachangamotishwa
na Mama Kanisa kuwa ni wataalam wa umoja, unaojidhihirisha katika maisha ya kiroho
kwa kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazoibuliwa katika mapambazuko ya Millenia
ya tatu ya Ukristo, ili kweli Kanisa liweze kuwa ni nyumba na shule ya umoja.
Ni
mwaliko kwa watawa kutoka katika ubinafsi wao, ili kwenda pembezoni mwa maisha ya
watu ndani ya jamii, kwani watu wengi bado wanangojea kusikia Habari Njema ya Wokovu,
sanjari na kusoma alama za nyakati ili kujibu kilio cha damu kutoka kwa watu wa nyakati
hizi, daima kwa kumsikiliza Roho Mtakatifu, ili kweli Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa
Duniani kiwe ni kipindi cha wongofu, neema na mabadiliko ya kweli, daima wakiwa na
ujasiri.
Haya ndiyo mambo msingi yanayopaswa kufanyiwa kazi katika Maadhimisho
ya Mwaka wa Watawa Duniani anasema Kardinali Joao Braz de Avis, Mwenyekiti wa Baraza
la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume katika mahubiri kwenye Ibada ya
kufungua Mwaka wa Watawa Duniani 2014 hadi mwaka 2016.