Viongozi wenye uchu wa madaraka watapambana na nguvu ya umma!
Rais Francois Hollande wa Ufaransa, amewaonya viongozi Barani Afrika wanaotaka kung'ang'ania
madarakani kwa kupindisha Katiba kwamba, watapambana na nguvu ya umma kama ilivyojitokeza
huko Burkina Faso, kwa kumng'oa kutoka madarakani Rais Blaise Compaore aliyetawala
kwa kipindi cha miaka 30 lakini bado alitaka kung'ang'ania madarakani. Tukio hili
liwe ni fundisho kubwa kwa viongozi wenye uchu wa madaraka. Rais Hollande ameyasema
haya mwishoni mwa juma, wakati alipokutana na viongozi wakuu wa nchi za Afrika Magharibi.
Katiba
za nchi nyingi Barani Afrika zimeweka vipindi viwili kwa Rais kuweza kukaa madarakani
na muda huu unapomalizika, awe radhi kung'atuka kutoka madarakani, lakini baadhi ya
Marais wamekuwa na kishawishi cha kutaka kupindisha Katiba za nchi ili waendelee kubaki
madarakani. Cameroon na Togo ni nchi ambazo zineonesha dalili za kutumbukia kwenye
kishawishi hiki.
Ufaransa inasema, itashikamana na nguvu ya umma kuwaondoa
madarakani viongozi wanaong'ang'ania kubaki madarakani kwa kupindisha Katiba na Sheria
za nchi, kwani kwa kufanya hivi, viongozi kama hawa wanahatarisha uhuru wa wananchi.