2014-11-30 11:11:43

Papa aanza siku ya tatu ya ziara yake Uturuki.


Jumapili hii, ikiwa ni siku ya tatu na ya mwisho ya ziara ya Papa Francisco nchini Uturuki ambako ametembelea miji ya Ankra na Istanbul, mapema asubuhi , ameifungua kwa maadhimisho ya Misa binafsi, katika jengo la Uwakilishi Papa la jijini Istanbul. Baada ya Misa, alikutana na Rabbi Mkuu wa Uturuki, Isak Haleva, kiongozi wa kiroho wa Jumuiya ya Wayahudi wapatao 25, 000, wanaoishi Uturuki nchi ya Waislamu wengi.Wayahudi wengi wanatajwa kuwa katika miji ya Istanbul na Izmir. Rabbi Haleva, pia aliwahi kukutana na Papa mstaafu Benedikto XVI alipotembelea Uturuki Novemba 30, 2006.

Na kisha Baba Mtakatifu Francisko, aliendelea na ratiba ya ziara yake kwa kutembelea Kanisa la Mtakatifu George , ambayo ni Makao Makuu ya Upatriaki wa Kiekumeni wa Constantinople, ambako alipokelewa na kukaribishwa Mwenyeji wake Patriaki Bartholomew I, na kuongozana pamoja ndani ya Kanisa kwa ajili ya kuanza Maadhimisho Ibada kwa mujibu wa Liturujia ya Maadhimisho ya Siku Kuu ya Mtakatifu Andrea Mtume.

Habari inasema, ilikuwa ni jambo la kuvutia kuona Baba Mtakatifu, alipokutana na Patriaki Bartholomeo I , aliinamisha kichwa chake kwa heshima kupokea baraka kutoka kwa Kiongozi wa Kanisa la Kiothodox, na walikumbatia kwa heshima ikionyesha urafiki mkubwa na imara kati yao. Pia inakumbukwa kwamba, mwaka jana, Patriaki Bartholomew I, alichukua hatua ya kipekee ya kuja Roma kwa ajili ya uzinduzi wa Utawala wa Kitume wa Papa Francisko, mara baada ya kuchaguliwa kuwa Papa, Mwezi Machi mwaka jana. Patriaki Bartholomew I, akishiriki katika khafla hiyo, alitoa mwaliko kwa Papa aitembelee Uturuki wakati wa kusherehekea sikukuu ya Mtakatifu Andrea, Jumapili Novemba 30.

Na imevutia jinsi Papa Francisco alivyozungukwa na Maaskofu waliovalia nguo nyeusi kutoka sehemu mbalimbali za dunia ya Kanisa la Kigiriki la Kiotodosi. Papa amezungumzia ahadi ya amani ya kweli ambayo Yesu alifanya na wanafunzi wake kwanza. Amesema, kama ilivyokuwa kwa Petro na Andrea, kukutana kwao kama waandamizi wa Petro na Andrea, ni neema na wajibu katika kutembea pamoja kama ndugu kwa matumaini ya Bwana Mfufuka. Na Patriaki, ameeleza kuwa ziara hii ya Papa Francisko, inaendelea kuwa tukio la kihistoria lililo jazwa na ishara za mazuri kwa siku za baadaye, kutembea pamoja katika njia ya kiekumeni. Ameonyesha tumaini lake kwamba, ziara hii ya Papa Francisco ni hatua nyingine muhimu katika barabara ya kuelekea kushinda mgawanyiko zamani, na kuwa na ubunifu mpya kwa ajili ya uwepo wa ushirikiano mpya kati ya wale wote wanaoweka imani yao kwa Mungu.








All the contents on this site are copyrighted ©.