Taarifa kwa umma kuhusu akaunti ya VIP Engineering and Marketing iliyopo katika
benki ya biashara ya Mkombozi: Utangulizi Taarifa hii inatolewa kwa umma kutokana
na ripoti mbalimbali zilizotolewa na baadhi ya vyombo vya habari mitandao ya kijamii
na taarifa iliyotolewa kwenye mjadala katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ufunguzi wa akaunti ya VIP engineering and Marketing (VIP)
Kampuni
ya VIP engineering and Marketing ni kampuni ambayo imesajiliwa kwa mujibu wa sheria
za Tanzania. Kampuni hii ilifungua akaunti katika benki ya biashara ya Mkombozi na
hivyo kuwa moja kati ya wateja wa benki. Benki ilijiridhisha na ilizingatia taratibu
zote za ufunguzi wa akaunti husika kwa kuzingatia sheria za nchi na kanuni zinazozitaka
benki kupata nyaraka muhimu kutoka kwa mteja wakati wa ufunguzi wa akaunti hiyo. Nyaraka
hizo ni pamoja na kuwepo kwa cheti cha usajili wa kampuni, kanuni za kampuni, idhinisho
la kampuni kumruhusu moja kati ya wanahisa wake kuendesha akaunti pamoja na picha
na hati ya kusafiria ya mhusika wa kuendesha akaunti hiyo. 2.0 Mauzo ya hisa
za VIP Kampuni ya VIP ilileta mkataba kwenye benki ya Mkombozi wa mauziano ya
hisa za asilimia 30 baina ya VIP na kampuni ya Pan Africa Power Solutions (PAP) ambazo
inamiliki katika kampuni ya IPTL. Mkataba huo ulisainiwa tarehe 19 Agosti, 2013. Bei
ya asilimia 30 ya hisa hizo ilikuwa ni dola za Marekani milioni 75. Katika kifungu
namba 2.4 cha mkataba wao kinaelekeza fedha za mauzo ya hisa zilipwe kwenye akaunti
ya VIP iliyopo benki ya Mkombozi. Mkataba huo wa mauziano ya hisa baina ya kampuni
hizi mbili ulitambuliwa na hukumu ya Mahakama Kuu ya Tanzania iliyotolewa na Jaji
J.H.K Utamwa tarehe 5 Septemba, 2013.
Mchakato wa kulipa
kodi ya serikali
Benki ilitambua kwamba katika mauziano hayo ya hisa ni
lazima kodi ya Serikali ilipwe na hivyo iliizishauri pande zote mbili kupeleka mkataba
husika katika ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kufanyiwa makadirio ya
kodi husika. Tarehe 20 Januari, 2014 TRA iliiandikia barua kampuni ya VIP na nakala
ya barua hiyo kuletwa kwenye benki ya Mkombozi. Katika barua hiyo TRA iliitaarifu
kampuni ya VIP kuwa makadirio ya kodi yatokanayo na mauzo ya hisa ni shilingi 38,186,584,322.00
ikiwa ni kodi ya mauzo ya hisa ya asilimia 30 za mauzo ya hisa kutoka VIP kwenda kwa
PAP.(Capital gains and stamp duty). TRA pia iliiagiza benki ya Mkombozi kuhakikisha
kuwa inalipa kodi hiyo kwa niaba ya VIP mara tu fedha zitakapoingia kwenye akaunti
yake.
Malipo ya kodi ya shilingi 38,186,584,322.00 yalilipwa TRA kwenye akaunti
11120100 iliyopo katika Benki Kuu ya Tanzania na TRA ilikiri kupokea kodi hiyo kwa
barua yake yenye kumbukumbu namba 3-4/100/100/223/4 ya tarehe 24 Januari, 2014.
Ufafanuzi wa mambo mbalimbali
4.1 Benki ya mkombozi kuhusika
katika kusafisha fedha chafu Fedha zote zilizoingizwa kwenye akaunti ya VIP iliyopo
kwenye benki ya Mkombozi zilitokana na mauziano ya hisa kati ya VIP na PAP kwa mkataba
uliotambuliwa na Mahakama Kuu ya Tanzania. Chanzo cha malipo hayo ni kuhamisha fedha
kutoka kwenye akaunti ya PAP iliyopo katika benki ya Stanbic na kuingizwa kwenye akaunti
ya VIP iliyopo katika benki ya Mkombozi. Fedha hizo zilihamishwa katika mafungu mawili.
Fungu la kwanza ilikuwa ni shilingi 73,573,500,000.00 zilihamishwa kwa njia ya TISS
kwa kumbukumbu namba 000000050720 ya tarehe 23 Januari, 2014 na fungu la pili ni dola
za Kimarekani 22,000,000.00 zilihamishwa kwa TISS kwa kumbukumbu namba 000000050812
ya tarehe 23 Januari, 2014. Malipo mengine ya asilimia kumi ya mauzo ya hisa yalilipwa
kwenye akaunti ya Mkombozi iliyopo Benki Kuu ya Tanzania. Kutokana na mchakato huo
benki ya Mkombozi ilijiridhisha kuwa fedha hizo ni malipo halali na siyo fedha chafu.
Benki ya Mkombozi haijihusishi na utakasishaji wa fedha chafu na haramu katika uchumi
wa Tanzania.
4.2 Malipo yatokanayo na akaunti ya VIP Malipo toka
kwenye akaunti ya mteja hufanywa kutokana na maelekezo ya mteja. Benki ikishajiridhisha
kuwa fedha ya mteja ni halali na ipo kwa mujibu wa sheria na hamna zuio lolote toka
katika mahakama hapa nchini hutekeleza malipo kwenye akaunti ya mteja kutokana na
maelekezo yake. Benki ilijiridhisha kuwa malipo yote yaliyofanywa kutoka kwenye akaunti
ya VIP ni halali kwa kuwa chanzo cha pesa hizo ilikuwa ni halali kutokana na mauzo
ya hisa na ulipwaji wa kodi ya Serikali kama ilinyoelezwa hapo juu. Kutokana na sababu
hiyo benki haikuwa na shaka juu ya malipo hayo.
4.3 Malipo taslimu kwa wateja
na kubeba fedha kwenye viroba, mifuko ya rambo na magunia. Benki inatoa tamko
kuwa malipo yote yaliyofanywa katika akaunti ya VIP yalilipwa kupitia akaunti za walipwaji.
Hakuna fedha zilizolipwa taslimu kwa wateja na kubebwa kwenye viroba au magunia kama
ilivyoripotiwa Bungeni. Pesa iliyotoka kwenye akaunti ya VIP tarehe 6 Februari, 2014
kiasi cha shilingi 3,314,850,000.00 ililipwa kwenye akaunti nane za wateja tofauti
na siyo kubebwa kwenye viroba au magunia. Na zile zilizotoka toka benki ya Stanbic
zilizotajwa hapo juu zilitumwa kwa njia ya TISS na siyo kubeba kwenye magunia au
viroba. 4.4 Malipo kwa mfanyakazi wa benki ya Mkombozi Gazeti la Mawio la
tarehe 20-26, Novemba, 2014 tolea namba 0122 liliandika kuwa mwanasheria wa benki
ya Mkombozi ajulikanaye kwa jina la Rweyengeza Alfred alipokea malipo toka akaunti
ya VIP ya shilingi milioni 40.2. Benki inatoa tamko kuwa haina mfanyakazi anayetambuliwa
kwa jina hilo na wala hakuna mfanyakazi yeyote wa benki aliyelipwa fedha toka kwenye
akaunti ya VIP. Wito kwa umma
Benki ya Mkombozi
inachukua fursa hii kuwatarifu wateja wake na umma kutopotoshwa na taarifa au tuhumma
zilizofafanuliwa hapo juu na kuwataka wateja wake wote kutokuwa na hofu yeyote kwani
benki ipo imara na inafanya kazi kwa kufuata misingi ya sheria, taratibu na kanuni
zilizowekwa na Benki Kuu ya Tanzania. Benki inawataarifu wateja wake na Watanzania
kwa ujumla kutoyumbishwa na tuhumma hizo ambazo hazina ukweli ndani yake na badala
yake waitumie benki yao kwa shughuli za maendeleo ya nchi yetu. Pamoja tunajenga nchi
na uchumi wa nchi yetu.
Hitimisho
Benki ya
biashara ya Mkombozi haijihusishi na haitajihusisha na utakasishaji wa fedha chafu.
Imetolewa na: MKURUGENZI MTENDAJI BENKI YA BIASHARA YA MKOMBOZI