Misimamo mikali ya kiimani na uhalifu kwa jina la kidini ni mambo ambayo hayawezi
kukubalika!
Majadiliano ya kidini kati ya Kituo cha Majadiliano na utamaduni wa dini ya Kiislam
na Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini, yaliyokuwa yanafanyika mjini Teheran
kwa kuongoza na kauli mbiu "Wakristo na Waislam katika majadiliano kwa ajili ya mafao
ya kijamii" umehitimishwa kwa washiriki kutoa tamko la pamoja linalopongeza juhudi
ambazo zimefikiwa hadi sasa katika kujenga na kuimarisha mahusiano kati ya pande hizi
mbili.
Dr. Abuzar Ibrahimi Turkaman aliongoza ujumbe kutoka upande wa waamini
wa dini ya Kiislam na Kardinali Jean Louis Tauran, Rais wa Baraza la Kipapa la majadiliano
ya kidini, aliongoza ujumbe kutoka Vatican. Mkutano huu wa siku mbili umepongeza jitihada
za makusudi baina ya waamini kutaka kufahamiana zaidi na hatimaye kujenga jamii yenye
amani, upendo na mshikamano.
Wajumbe hawa wamelaani kwa kauli moja misimamo
mikali ya kiimani pamoja na vitendo vyote vya uhalifu kwa misingi ya kidini, kuwa
ni mambo ambayo hayawezi kukubalika. Wajumbe hawa watakutana tena mjini Roma kunako
mwaka 2016, lakini mwaka 2015 utakuwa na vikao vya maandalizi ya pamoja.