Serikali ya Tanzania imesema kuwa VICOBA ni taasisi binafsi inayomilikiwa na wananchi
wenyewe vikiwa ni miongoni mwa tasisi ndogo za kifedha ambazo ni za kibinafsi na huanzishwa,
kuendeshwa na kusimamiwa ama kijijini, kitongojini na hata kwenye kata.
Hayo
yamebainishwa Ijumaa tarehe 28 Novemba 2014 Bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri wa
Fedha Mwigulu Nchemba alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Rungwe Magharibi Prof.
David Mwakyusa (CCM) ambaye alitaka kujua kama Serikali inatambua VICOBA kama mkombozi
wa wanyonge. Mwigulu amefafanua kuwa taasisi hizo zimo kwenye sekta ya fedha isiyorasmi
na zinatoa huduma za kifedha mijini na vijijini.
“Uwepo wa taasisi hizi,
umewezesha kufikisha huduma za kifedha kwa wananchi waliombali na huduma za sekta
rasmi ya fedha na hivyo kuwa mkombozi wa wanyonge” alisema mwigulu. Aidha, kwa kutambua
suala hilo, ili kusaidia na kuimarisha taasisi hizo, Mwigulu amesema kuwa Serikali
baada ya kupata ushauri kutoka kwa Mshauri Mwelekezi wa masuala ya uchumi na tafiti
za kijamii, inafanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Taasisi ndogo za huduma ya fedha
ya mwaka 2000 ili kuihuisha iweze kukabili na kuzingatia mabadiliko na maendeleo yanayojitokeza
katika sekta hiyo.
Vilevile Mwigulu amesema kuwa Serikali inakamilisha
uhuishaji wa sera ya taasisi ndogo ndogo za kifedha ambapo hatua inayofuata ni kuandaa
mapendekezo ya muswada ambayo yatapelekwa Baraza la Mawaziri mara baada ya kupata
idhini na maelekezo ya Baraza hilo na muswada huo utafikishwa bungeni. Taasisi ya
VICOBA ilianzishwa nchini mwanzoni mwa miaka ya 2000, ambapo imekuwa na manufaa kwa
wananchi wengi wenye kipato cha chini hususan wanawake waishio vijijini wamefanikiwa
kuboresha kipato chao na maisha yao kwa ujumla kwa kujiunga na taasisi hiyo.