Siku ya mshikamano wa kimataifa na Wananchi wa Palestina
Bado kuna kinzani na migogoro mikubwa kati ya Palestina na Israeli, kiasi cha kugumisha
mchakato wa kutafuta amani hasa kwenye Ukanda wa Ghaza, changamoto kwa pande hizi
mbili kusitisha vita na kuendeleza majadiliano ya amani na upatanisho.
Umoja
wa Mataifa unalaani mashambulizi ya makombora yanayofanywa na Hamas dhidi ya raia
wa Israeli, mambo yanayosababisha mateso na mahangaiko makuba kwa watu wasiokuwa na
hatia. Mashambulizi yaliyofanywa na Israeli huko Palestina yamesababisha maafa makubwa
kwa watu na mali zao, mwaliko kwa Israeli kuwajibika barabara katika maamuzi yake
sanjari na kulinda haki msingi za binadamu kimataifa.
Hii ni sehemu ya ujumbe
kutoka kwa Bwana Ban Ki-Moon, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, katika maadhimisho
ya Siku ya Kimataifa ya Mshikamano na Wapalestina, inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo
tarehe 29 Novemba. Amani na utulivu anasema Katibu mkuu, vinategemea kwa namna ya
pekee kabisa utashi kutoka kwa pande zote mbili; kwa kuheshimu sheria za kimataifa
sanjari na Israeli kuacha ujenzi wa makazi katika maeneo ya Palestina.
Katibu
mkuu wa Umoja wa Mataifa anawakumbuka kwa namna ya pekee, wakimbizi kutoka Palestina
wanaoishi kwenye Ukanda wa Ghaza na kwingineko. Anawapongeza wafanyakazi wa Umoja
wa Mataifa wanaowahudumia wakimbizi huko Mashariki ya Kati pamoja na kusaidia mchakato
wa ujenzi wa Gaza, ingawa hali bado si shwari sana huko Yerusalem. Hapa kuna haja
kwa pande hizi mbili kuheshimiana na kuacha kuendeleza ujenzi usio halali kwenye makazi
ya Wapalestina.
Mgogoro kati ya Palestina na Israeli utamalizika, ikiwa kama
kutakuwepo na utashi wa kisiasa unaozingatia misingi ya usawa, majadiliano pamoja
na kusimamia maafikiano yaliyokwisha kutolewa na Umoja wa Mataifa. Waisraeli na Wapalestina
wanategemeana na hivyo wanapaswa kuishi kwa kuvumiliana kwani wanahitajiana. Siku
ya mshikamano na Wananchi wa Palestina iwatie shime viongozi wa Israeli na Palestina
kuachana na falsafa ya kulipizana na kisasi na kujikita katika mchakato wa ujenzi
misingi ya haki na amani.