2014-11-28 15:19:10

Papa aanza ziara ya kitume ya Kimataifa ya sita Uturuki


Papa Francisko, anatimiza maneno yake kwamba Kanisa, lisibaki limejifungia ndani lenyewe bali litoke nje na kukutana na watu. Kwa nia hiyo, mapema ijumaa hii, aliondoka Vatican na kuelekea Uturuki, ikiwa ni ziara yake Kitume ya Kimataifa ya Sita, ambako atakaa kwa muda wa siku tatu, Ijumaa 28-30 Novemba 2014.
Papa anafanya ziara hii kwa mwaliko toka pande zote mbili, Rais wa Jamhuri ya Uturuki, Mheshimiwa Rais Recep Yayyip Erdogan na Kiongozi Mkuu wa Kiroho, Kanisa la Kiotodosi la Upatiaki wa Constatinople, Patriaki Bartholew, kwa ajili ya kushiriki katika Siku Kuu ya Mtakatifu Andrea, mwanafunzi wa Yesu aliyeanzisha Kanisa la Mashariki. Siku Kuu inayo heshimiwa sana Kanisa la Kiotodosi. Kwa kuwa Papa anafanya ziara hii akiitikia mialiko kutoka pande mbili tofauti, hivyo anatembelea Uturuki katika mtazamo mpana wa Kisiasa na pia kwa nia za kidini. Hivyo Papa anakutana na wote viongozi wa kisiasa na viongozi wa kidini.

Baba Mtakatifu aliianza ziara hii majira ya saa tatu kwa ndege ya Shirika la ltalia katika Uwanja wa Fiumicino Roma hadi Ankra Uturuki, mwendo wa saa tatu , akipita katika anga la Italia, Albania , Ugriki na Uturuki. Akipita katika anga za mataifa hayo alipeleka salaam kwa Wakuu wa Nchi katika mataifa hayo, akijulisha uwepo wake .
Kwa Rais wa Italia, Giorgio Napolitano , amesema, katika muda huo, anaianza safari yake ya kuelekea Uturuki , kwa ajili ya kukutana na kuzungumza na tamaduni mbalimbali , kwa lengo la kuimarisha njia ya kutembea pamoja katika umoja wa Wakristo na kwa ajili ya kutolea sala na maombi kwa kushirikiana pamoja na wapendwa katika imani wake kwa waume. Hivyo kwa furaha pia alitoa salaam zake za dhati kwa Rais Giorgio, na kwa taifa lote la Italia ,akiwa amejawa na ma kwa tumaini makubwa kwamba, kiroho wataongozana nae kwa ajili ya ujenzi wa maendeleo yao ya kiroho, kwa manufaa ya raia na jamii yote ya Italia.
Na wakati akipita katika Anga la Albania, alitoa salaam zake kwa Rais Bujar Nishani, na wananchi wa Albania , ambamo alishukuru kwa kumruhusu kupita katika anga hilo wakati akielekea Uturuki. Aliikumbuka pia ziara yake aliyoifanya nchini Albania, alirudia kwa mara ingine kuliombea taifa hilo Baraka za Bwana wa amani na ustawi kwa ajili ya taifa zima.

Na alipoingia katika anga ya Ugriki, vivyo hivyo alipeka salaam kwa Rais wa Jamhuri ya Ugriki, Rais Karolos Papoulias, na kwa watu wote wa Ugriki akiwa njiani kuelekea Uturuki,. Alimwomba Bwana alibariki taifa hilo na wingi wa amani na ustawi.

Baba Mtakatifu alitua katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Esemboga Ankra Uturuki majira ya saa saba kwa majira ya Uturuki na kupokelewa uwanjani hapo na Nunsio wa Kitume na Waziri Mkuu na Mkuu wa jeshi na Meya wa mji wa Ankra na viongozi wake wengine wakuu wa Kikanisa na kiserikali.
Mji wa Ankra unafahamika kama mji Mkuu wa Kisiasa , wa tangu mwaka 1923, wakati wa kuzaliwa rasmi taifa la Uturuki. Una wakazi wapatao milioni 4.4. Ni mji mashuhuri wenye kuwa na jengo la Makumbusho ya historia ya tangu karne ya tatu A.D na pia sehemu ya ukuta wa tangu miaka ya 620, ambavyo leo hii viko chini ya UNESCO.
Baada ya mapokezi ya uwanjani, Papa alitembelea jengo la Makumbusho la Ataturk, lililojengwa kati ya mwaka 1944 hadi 1953, ambalo linahifadhi masalia ya Mustafa Kemal “Ataturk” anayefahamika kama “Baba wa Uturuki”, Mwanzilishi wa na Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Uturuki (1923 38). Ni kiongozi anayekumbukwa kwa ushupavu wake, uliowezesha mabadiliko makubwa kitaifa, kutoka taifa la kiislam na kuwa taifa huria lisilo la kidini baada ya kwa kuuangusha utawala wa mabavu wa Kiislamu wa Ottoman, uliokuwa ukifuata sharia za Kiislamu.
Papa atakuwa uturuki hadi siku ya Jumapili 30 Novemba.








All the contents on this site are copyrighted ©.