2014-11-28 12:02:44

Hija ya Papa Francisko nchini Uturuki, lengo ni kuimarisha: majadiliano na udugu


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anasema, hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Uturuki kuanzia tarehe 28 hadi tarehe 30 Novemba, 2014 ni kutaka kuimarisha na kudumisha majadiliano ya Kiekumene kati ya Wakristo; udugu kati ya watu pamoja na kuendeleza mchakato wa haki na amani huko Mashariki ya Kati.

Baba Mtakatifu katika hija hii ya kitume, wataadhimisha kwa pamoja Siku kuu ya Mtakatifu Andrea na kutia sahihi tamko la pamoja kuhusu majadiliano ya kiekumene, mwendelezo wa tamko lililotiwa sahihi wakati Baba Mtakatifu Francisko alipofanya hija ya kichungaji katika Nchi Takatifu, kunako mwaka 2014. Lengo ni kuimarisha misingi ya upendo, udugu na mshikamano, pamoja na kusimama kidete kulinda na kutetea: haki na amani sanjari na uhuru wa kuabudu huko Mashariki ya Kati, ambako kuna idadi kubwa ya Wakristo wanaoendelea kuteseka na kunyanyasika kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.

Ili amani ya kweli iweze kupatikana huko Mashariki ya Kati kuna haja kwa pande zote zinazohusika kuweka silaha chini ya kuanza kujikita katika majadiliano yanayojikita katika ukweli, uwazi na upatanisho; lakini ukweli wa mambo mchakato wa amani unaendelea kupambana na kinzani nyingi kiasi hata cha kuwakatisha wananchi tamaa ya kupata amani ya kweli.

Kardinali Parolin anasea, dhamana na utume wa Kanisa ni kuendelea kuwa ni sauti ya kinabii kwa watu wanaoteseka na kunyanyasika; watu wanaolazimika kuyakimbia makazi yao kwa kuhofia usalama wa maisha yao, ili Jumuiya ya Kimataifa iweze kuchukua hatua zinazofaa ili kuwalinda watu hao. Kanisa kwa kutumia Mashirika yake ya misaada linaendelea kuwahudumia wakimbizi na wote wanaohitaji huduma bila ya ubaguzi. Kipindi cha baridi, hali itakuwa ni mbaya sana, kumbe, Kanisa linaendelea kukazia umuhimu wa watu kurejea tena kwenye makazi yao.

Kanisa Katoliki nchini Uturuki ni kundi dogo ambalo nalo limepitia katika majaribu makubwa, lakini bado lipo na linaendelea kutoa ushuhuda wa utume wake kwa njia ya majadiliano ya kidini na Waamini wa dini ya Kiislam.







All the contents on this site are copyrighted ©.