Askofu mkuu Josè Rodriguez Carballo, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Mashirika
ya kitawa na kazi za kitume anasema kwamba, maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani
yataanza kutimua vumbi hapo tarehe 30 Novemba 2014, Jumapili ya kwanza ya Majilio,
kipindi cha matumaini na kuhitimishwa rasmi tarehe 2 Februari 2016, Siku ya Watawa
Duniani.
Hiki ni kipindi
chenye utajiri mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kuangalia umuhimu na mchango
wa Watawa katika mchakato wa Uinjilishaji mpya; fursa zilizopo na changamoto mbali
mbali zinazowakabili watawa sehemu mbali mbali za dunia.
Maadhimisho ya Mwaka
wa Watawa Duniani ni mwendelezo wa mchakato wa hija ya maisha ya Kanisa katika mapambazuko
ya Millenia ya Tatu ya Ukristo, changamoto iliyofanyiwa kazi kwa namna ya pekee na
Mtakatifu Yohane Paulo II, kwa kuangalia changamoto zilizopita, hali ya sasa ya maisha
na utume wa Kanisa na kujiwekea mikakati ya shughuli za kichungaji kwa siku za usoni.
Kanisa linapenda kuyaangalia maisha na utume wa watawa ndani ya Kanisa tangu baada
ya maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.
Hiki ni kipindi cha kumkshukuru
Mungu kwani kumekuwepo na maendeleo pamoja na mchango mkubwa uliotolewa na watawa
ndani ya Kanisa, ili kwa mara nyingine tena watawa waweze kumwimbia Mwenyezi Mungu
utenzi wa sifa na shukrani kwa kusema, “tazama inavyopendeza kuwa mtawa ili kumfuasa
Yesu na kuwatumikia jirani bila ya kujibakiza”!
Kwa njia hii, Mama Kanisa
anapenda kuimarisha mikakati ya shughuli za kichungaji katika kukuza na kuimarisha
miito ya kitawa ndani ya Kanisa. Hapa Kanisa linaialika Familia ya Mungu kutafakari
juu ya “Maisha ya kitawa: injili; Unabii na Matumaini ndani ya Kanisa”.
Maadhimisho
haya katika ngazi ya kimataifa anasema Askofu mkuu Carballo ni kuanzia tarehe 22 hadi
tarehe 24 Januari 2015, maadhimisho haya yatakuwa na sura ya kiekumene. Katika maadhimisho
ya Siku kuu ya Pasaka kuanzia tarehe 8 hadi tarehe 11 Aprili, 2015 kutafanyika kongamano
la walezi. Tarehe 23 hadi tarehe 26 Septemba kutafanyika kongamano la watawa vijana,
watakaowasha moto wa Injili mjini Roma kwa kuwashirikisha vijana wenzao uzuri wa kutangaza
Injili katika maisha ya kitawa na kazi za kitume.
Mwishoni mwa Januari 2016
kutafanyika kongamano la watawa na mashirika ya kazi za kitume kwa kuwashirikisha
Marais wa Mashirikisho ya Mabaraza ya Mashirika ya Kitawa na kazi za kitume kutoka
sehemu mbali mbali za dunia. Katika matukio yote haya kunatarajiwa uwepo wa Baba Mtakatifu
aidha kwa kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu au kwa njia ya kukutana na kuzungumza
na makundi haya.
Baraza la Kipapa la Mashirika ya kitawa na kazi za kitume
linasema kwamba, maadhimisho ya Mwaka wa watawa Duniani ni tukio litakaloyashirikisha
pia Mabaraza mengine ya kipapa, Shirikisho la wakuu wa Mashirika ya Kitawa pamoja
na Vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa.
Askofu
mkuu Carballo anasema, mkutano mkuu wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na
kazi za kitume utafanyika kuanzia tarehe 25 hadi tarehe 29 Novemba 2014 kwa kuongozwa
na kauli mbiu “Divai Mpya katika Viriba Vipya”, ni mwaliko wa kusikiliza hija ya
maisha ya watawa mintarafu mwongozo wa Roho Mtakatifu, changamoto kwa watawa kuendelea
kuwa waaminifu katika karama za mashirika yao sanjari na kusoma alama za nyakati.
Maadhimisho
ya Mwaka wa Watawa Duniani ni tukio la Kikanisa, kumbe, Makanisa mahalia kwa kushirikiana
kwa karibu zaidi na watawa wanaweza kujipangia ratiba itakayowawezesha kuadhimisha
Mwaka wa Watawa Duniani kwa ari na moyo mkuu.
Askofu mkuu Carballo anasema
kwamba, kongamano la watawa mintarafu mwelekeo wa kiekumene ni mwaliko wa kujichotea
utajiri mkubwa unaofumbatwa katika maisha ya kitawa na kazi za kitume kutoka kwenye
Makanisa ya Mashariki. Hapa ni mahali pa kufanya upembuzi yakinifu ili kuibua utajiri
huo ambao pia unahitajika kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa zima, ili kuendeleza
majadiliano ya kiekumene yanayojikita katika maisha ya kiroho. Watawa wanaweza kutoa
mchango mkubwa katika utekelezaji wa dhamana hii, ili wote wawe wamoja chini ya mchungaji
mmoja yaani Yesu Kristo!
Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuhimiza umuhimu
wa majiundo makini kwa Makleri na watawa ndani ya Kanisa. Mwaka wa Watawa Duniani
itakuwa ni fursa ya kupembua kwa kina na mapana mikakati ya malezi kwa kuimarisha
na kuboresha pale itakapoonekana inafaa zaidi. Ni mwaka unaomwangali mtawa kama binadamu
kamili katika mahitaji yake msingi: kiroho na kimwili, mitarafu mafundisho ya Mababa
wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.
Watawa hawana budi kujenga na kuimarisha
mahusiano yao na Yesu Kristo kwa njia ya Sakramenti, Tafakari ya Neno la Mungu linalomwilishwa
katika imani tendaji. Kwa maneno mafupi, watawa wanaalikwa kuwa ni mashahidi wa Kristo
na Kanisa lake kwa njia ya maisha na utume wao. Maisha ya kijumuiya ni kati ya mambo
ambayo yataendelea kuwekewa msisitizo wa pekee, ili kujenga na kudumisha upendo, umoja
na udugu katika Kristo.
Maisha ya kitawa hayana budi kukumbatia na kumwilisha
Mashauri ya Kiinjili: Yaani: utii, ufukara na useja, kama kielelezo makini cha unabii
na mwaliko wa kuuamsha ulimwengu, kama alivyokazia Baba Mtakatifu Francisko alipokutana
na kuzungumza na Wakuu wa Mashrika ya Kitawa, hii ikawa ni chemchemi ya maadhimisho
ya Mwaka wa Watawa Duniani.
Ni changamoto na mwaliko kwa Mashirika ya kitawa
na kazi za kimissionari sehemu mbali mbali za dunia kuhakikisha kwamba, yanamwilisha
karama na utume wao mahali wanapoishi na kufanya kazi kwa kutambua kwamba, utamadunisho
wa karama za Mashirika ya kitawa na kazi za kitume bado ni changamoto pevu kwa mashirika
mengi!
Baraza la Kipapa la Mashirika ya kitawa na kazi za kitume linataka kuanzisha
majiundo awali na endelevu kwa watawa kwa njia ya mitandao ya kijamii. Watawa wanaalikwa
kuanzisha mnyororo wa sala kwa ajili ya kuliombea Kanisa, maisha ya kitawa na ulimwengu
katika ujumla wake. Baraza pia linapitia nyaraka mbali mbali zinazogusia moja kwa
moja maisha ya kitawa na kazi za kitume ndani ya Kanisa.
Kwa ufupi anasema
Askofu mkuu Josè Rodrguez Carballo, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya
Kitawa na Kazi za Kitume, Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani ni moto wa kuotea
mbali!
Imeandaliwa na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili
ya Radio Vatican.