2014-11-25 07:31:32

Uhuru wa kidini na haki msingi za binadamu ni mambo msingi katika kudumisha amani!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 24 Novemba 2014 amekutana na kuzungumza na Rais Abdel Fattah Alsisi, Rais wa Misri, ambaye baadaye amekutana na kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican. Viongozi hawa katika mazungumzo yao, wamebadilishana mawazo kuhusu hali ilivyo kwa sasa nchini Misri, kwa kuonesha mshikamano wa Kanisa kwa wananchi wote wa Misri katika kipindi hiki cha mabadiliko ya kisiasa.

Baba Mtakatifu na mgeni wake wamezungumzia pia umuhimu wa Katiba mpya ya Misri katika mchakato wa kulinda na kudumisha haki msingi za binadamu na uhuru wa kidini, ili kusaidia ujenzi wa dhamiri nyofu zinazoheshimu na kuthamini amani na utulivu kati ya watu, huku wakiendeleza majadiliano ya kidini.

Viongozi hawa wamepembua pia baadhi ya masuala ya kimataifa hasa nafasi na dhamana ya Misri katika mchakato wa kutafuta amani na utulivu huko Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika. Viongozi hawa wanaamini kwamba, majadiliano ya kina ndiyo njia pekee inayoweza kuleta ufumbuzi wa kudumu katika maeneo yenye migogoro ya kivita na kinzani za kijamii; mambo yanayopelekea watu wengi kupoteza maisha yao!







All the contents on this site are copyrighted ©.