Mchakato wa mabadiliko mjini Vatican umefikia hatua nzuri!
Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, 24 Novemba 2014 amekutana na kuzungumza na Wakuu
wa Mabaraza ya Kipapa mjini Vatican, ili kufafanua kwa kina na mapana hatua ambazo
zimekwishafikiwa katika mchakato wa kufanya mabadiliko ya kina kwenye Makao makuu
ya Vatican kama walivyopendekeza Makardinali katika mikutano yao elekezi kabla ya
uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, uliofanyika mwezi Machi, 2013.
Padre
Federico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican anasema, mkutano huu umedumu kwa takribani
masaa matatu na hotuba ya ufunguzi imetolewa na Askofu Marcello Semeraro, Katibu wa
Baraza la Makardinali, lililoundwa na Baba Mtakatifu Francisko, mwaka 2013 ili kumsaidia
katika kuongoza Kanisa la Kristo pamoja na kupitia upya mkakati wa kiuchungaji uliobainishwa
kwenye Waraka wa Kichungaji, "Pastor bonus" Mchungaji mwema.
Askofu Semeraro
amefafanua mambo msingi yanayopaswa kufanyiwa kazi katika mchakato wa mabadiliko ya
Makao makuu ya Vatican. Wakuu wa Mabaraza ya Kipapa na vitengo mbali mbali wamechangia
mawazo na mang'amuzi yao na kwamba, Baraza la Makardinali linatarajiwa kufanya vikao
vyake kuanzia tarehe 9 hadi tarehe 11 Desemba 2014 hapa mjini Vatican.
Na Padre
Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.