2014-11-25 08:35:58

Kardinali Robert Sarah ateuliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa Baraza la Kipapa la Ibada na Sakramenti za Kanisa


Baba Mtakatifu Francisko amemteua Kardinali Robert Sarah kuwa Mwenyekiti mpya wa Baraza la Kipapa la Ibada na Sakramenti za Kanisa. Kabla ya uteuzi huu, Kardinali Robert Sarah alikuwa ni Rais wa Baraza la Kipapa linaloratibu misaada ya Kanisa Katoliki, Cor Unum. Anachukua nafasi ya Kardinali Antonio Canizares Llovera aliyeteuliwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Valencia, Hispania.

Kardinali Robert Sarah alizaliwa kunako Mwaka 1945 huko Guinea Conakry. Baada ya kupewa Daraja Takatifu la Upadre, alitumwa na Askofu wake kwa ajili ya masomo ya juu kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian, huko "akajichimbia" katika masomo ya Sayansi ya Maandiko Matakatifu na baadaye akajiendeleza zaidi kwenye Chuo cha Sayansi ya Maandiko Matakatifu kilichoko mjini Yerusalem na huko akajipatia Shahada ya Uzamili katika Sayansi ya Maandiko Matakatifu.

Baada ya masomo yake alirejea nchini mwake na kupangiwa kazi mbali mbali za kitume kama Paroko na Gombera wa Seminari ndogo ya Yohane XXIII, hadi mwaka 1979 Mtakatifu Yohane Paulo II alipomteuwa kuwa Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, utume alioufanya kwa kipindi cha miaka tisa, hadi tarehe 7 Oktoba 2010, Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI alipomteua kuwa Rais wa Baraza la Kipapa linaloratibu misaada ya Kanisa Katoliki, Cor Unum na baadaye tarehe 20 Novemba 2011 akateuliwa kuwa Kardinali.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican







All the contents on this site are copyrighted ©.