2014-11-24 16:10:46

Miasha ya Kitawa ndani ya Kanisa


Jumapili ya kwanza ya kipindi cha majilio, utaanza rasmi mwaka wa Maisha yaliyowekwa Wakfu, maisha ya kitawa, kama ilivyokwisha tangazwa na Papa Francisko, kwamba utaanza Novemba 29, 2014 hadi tarehe 2 Februari, 2016, ambayo ni Siku ya Watawa Duniani..

Baba MtakatifuFrancisko, awali katika hotuba zake , aliutaja mwaka 2015 uwe ni mwaka wa maisha yaliyo wekwa wakfu , kwa nia kwamba , watu wote walio yatolea maisha yao katika wakfu wa kumtumikia Mungu na Kanisa, wanawake na wanaume, waweze kukuza ufahamu juu ya nia na majitoleo ya maisha yao kwa Kristo na mwili wake Kanisa. Maamuzi yao ya kuitikia wito huu wa kulitumikia kanisa ni muhimu katika uhai na kazi za Kanisa. Mwaka huu wa watawa unaongozwa na kaulimbiu: Maisha yoliyowekwa Wakfu ndani ya Kanisa; Unabii na Matumaini ya kijamii.

Kwa hiyo ni matazamio ya Mama Kanisa kwamba, maadhimisho ya mwaka huu, yataweza kuongeza zaidi mwitikio wa wanaume na wanawake, kujibu kwa ukarimu na uaminifu, wito wa kufuata njia ya maisha yaliyowekwa wakfu. Katika mwaka huu pia waamini wanaombwa kuongeza sala na maombi kwa Bwana, ili kwamba wengi waweze kuisikia sauti inayowaita katika utumishi huu na pia waliokwisha itikia mwaliko huu wapate kutumikia kwa unyenyekevu, uvumilivu na uaminifu, na kuwa karibu zaidi na Mungu katika kufanya mapenzi yake.

Mababa wa Kanisa, wakati wa Baraza Kuu la Pili la Vatican, wakitafakari wingi wa karama katika kanisa,waliona kwamba, hakuna sababu ya kuogopa wingi wa uwepo wa mashirika ya watawa, kwa kuwa wingi wa karama ni neema kwa Kanisa, maana wote wameitwa na Mungu kuitumikia Injili, katka uaminifu wa kuyaweka wakfu maisha, na nadhiri za kuuishi umasikini kama Bwana Yesu ilivyosema katika Injili ya Matayo “mbweha wana pango na ndege angani wana viota, lakini mwana wa Adamu hana pa kulaza kichwa chake ( Mt 8:20;lk 9:58) aliwakomboa wanadamu na kutakasa kwa njia ya utii wake mpaka kufa msalabani. Mababa wa Kanisa walieleza hilo katika kutazama hali halisi kwamba, kuna mashirika ya watawa zaidi ya 300 kwa watawa wanaume na mashirika zaidi ya 700 kwa watawa wa kike. Mababa wa Sinodi iwalimshukuru Mungu kwa ajili ya utakatifu na ukarimu wa wote , waliochagua maisha ya kidini , wake kwa waume, wana wa Kanisa, kwa kuwa yote ni Neema ya Mungu.

Aidha tunapotafakari juu ya mwaka huu wa Watawa, tunakumbuka , ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisco kwa Kongamano la Kimataifa la Taasisi za Maisha yaliyowekwa Wakfu na Mashirika ya Kitume katika Huduma ya Binadamu na Utume wa Kanisa , lililofanyika Machi 08-09 , 2014, katika Chuo Kikuu cha ANTONIANUM, Rome. Papa alisema, katika uso wa nyakati zetu, wenye kuwa na mabadiliko makubwa na ya haraka katika maendeleo ya mambo mengi, ni wazi matokeo yake yanajionyesha katika maisha ya watu. Katika uso wa uhakika wa wanaoishi wanaume na wanawake wa wakati wetu, wengi wanapambana na mambo yanayoleta udhaifu wa kiroho na mmomonyoko wa maadili kwa watu wengi, hasa vijana. Hivyo hali hii ni changamoto kwa jumuiya ya Kikristo.

Katika maono hayo, Ujumbe wa Papa Francisco ulihimiza kwamba, ni lazima na muhimu kwa Taasisi za Watawa na Vyama ya Maisha ya Kitume, kuwa mfano hai katika kushuhudia kanuni ya fadhila na mantiki ya zawadi ya upendo wa Kiinjili, kupata nafasi yake, katika shughuli za kiuchumi, kama karama za waanzilishi wengi wa taasisi namashirika ya kidini , walivyoonyesha hamu yao katika kuwa-zawadi, kupitia maisha wakfu, kutoa mchango wao halisi, kiuchumi, kijamii na kisiasa. Uaminifu katika karama za waanzilishi na urithi wa kiroho, pamoja na madhumuni ya kweli ya kila taasisi, inakuwa ni kigezo cha kwanza katika kutathmini utawala, usimamizi na utendaji wote wa shirika au taasisi katika ngazi yoyote ile. Asili ya karama, hutoa nguvu ya kudumisha uaminifu na huongeza moyo wa utume kwa ajili ya wote katika umoja wao.

Kwa hiyo Papa alisema, ni lazima kuwa macho ili kuhakikisha kuwa , Mashirika na Taasisi za Kanisa, zinasimamiwa na kuongozwa kwa uwazi, kulindwa na kuhifadhi kama kipaumbele, karama za kiroho, hata katika mwelekeo wa kiuchumi na ufanisi wake katika mapokeo yake ya utamaduni wa utawala wa taasisi, bila kuvumilia aina yoyote ya tabia inayotaka kuwa kinyume na karama za shirika na katika kuwa makini kwa matumizi mazuri ya rasilimali.

Kwa ajili Papa alitoa mwaliko kwa mashirika na taasisi zote za maisha yaliyowekwa wakfu , kuwa na muda wa kuchunguza utakatifu wa maisha yake kwa ajili ya kuleta upya chanya . Papa alifanya rejea kwa Mtumishi wa Mungu Paulo VI , ambaye wakati wa Mtaguso Mkuu wa Pili , alikumbusha haja ya kufanya upya na halisi mawazo Mkristo, mtindo mpya wa maisha ya Kanisa, kusikiliza maoni ya umma ndani na nje ya Kanisa, nia na haja ya kuona umaskini wa kiinjili na zaidi kutambua mahali ambapo, Injili inahitaji kuhubiriwa kwa ushujaa zaidi .

Papa Francisco, alizitaka Taasisi za Watawa na Vyama ya Maisha ya Kitume kuwa sauti ya kinabii na shuhuda mahiri aminifu kwa Kristo, ambaye yeye mwenyewe alikubali kuishi katika hali ya umasikini, na katika umasikini wake, binadamu anapata kutajirishwa na kupata heshima iliyo kuu kuliko zote, stahili ya kuitwa wana wa Mungu. Umaskini huu ni upendo na mshikamano, upendo wa kushirikiana kwa unyenyekevu katika hali zote, wakati wa furaha na hata katika harakati za kutafuta haki, na kuwa macho na miungu wanao tafuta kutia giza maana ya kweli ya maisha yaliyowekwa wakfu.

Papa ameasa kwamba, haisaidii kuwa maskini kinadharia. Umaskini unaotajwa ni ule unaogusa mwili wa Kristo, katika unyenyekevu wa kuhudumia maskini wa maskini, wagonjwa, watoto na wanyonge.

Kumbe tunaona wale wanao amua kuishi mtindo huu wa maisha yaliyo wekwa wakfu, wamehimizwa kuuishi upendo unao miminwa ndani mwao na Roho Mtakatifu, , kuishi zaidi na zaidi, kwa ajili ya Kristo na kwa ajili ya mwili wake ulio Kanisa. Ni maisha ya majitoleo yenye heshima kubwa katika kujiunga kwa mwamko wa miali ya moyo wa Roho Mtakatifu na Kristo katika njia ya maisha yote , na kwa namna hiyo, hiyohiyo , maisha ya kanisa yananufaika na utume wake na huzidi kuwa na nguvu.

Mpendwa msomaji, nasi sote kama walei wana wanakanisa, sote tunaalikwa, katika mwaka huu wa Watawa, kutembea pamoja nao, kuwasindikiza katika hija ya maisha yao kwa kutolea sala na maombi yetu kwa bidii zaidi, ili kwamba, nia ya Papa ya kwa ajili ya Maisha yaliyowekwa wakfu, uweze kuzaa matunda mengi mema kwa ajili ya utume wa Kanisa, ili kwamba, waweza kuwa karibu zaidi na Mungu. Tusali ili kwamba, mwaka huu wa Maisha yaliyowekwa Wakfu na uwezeshe Watawa wote, kurudi kwenye chemchemi za maisha ya Kikristo na roho ya mwanzilishi wa shirika, muda wote wa hija ya maisha yao, katika mazingira ya nyakati yaliyobadilika. Upya ufanyike chini ya msukumo wa Roho Mtakatifu na uongozi wa Kanisa, kama inavyotakiwa kutekelezwe kadiri ya kanuni zake msingi. Kanuni ya kwanza ikiwa ni kumfuata Kristo kwa kadiri ya Mafundisho Injili.

Tuombe ili kwamba , walioweka maisha yao wakfu, daima wasipungukiwe na hamu ya kuishi katika utaratibu wa maisha ya sala na utendaji amani katika kazi za maisha ya kawaida, kimwili na kisaikolojia , na kwa mujibu wa mahitaji ya kitume, na taratibu za kanisa mahalia, mazingira ya kijamii, na kwa mujibu wa kanuni na tabia ya kila shirika. Wanashirika wa shirika lolote wakumbuke kwamba waliitikia wito wa Mungu kwa kuweka nadhiri za zao kwa mujibu wa mafundisho ya kiinjili, ili kwamba wao wenyewe, wakiwa wamekufa kwa dhambi (taz. Rum 6:11), na pia wamekataa ulimwengu, wanaishi kwa ajili ya Mungu peke yake. Maisha yao yote yamekuwa kwa ajili ya kumtumikia Mungu, nayo ni aina ya pekee ya kujiweka wakfu ambao msingi wake imara umo katika wakfu wa ubatizo.Na T.J. Mhella







All the contents on this site are copyrighted ©.