2014-11-24 14:10:43

Kenya yalipiza kisasi dhidi ya Kikundi cha kigaidi cha Al Shabaab


Vikosi vya ulinzi na usalama nchini Kenya, mwishoni mwa juma vimefanya operesheni maalum dhidi ya Kikundi cha kigaidi cha Al Shabaab, kilichodai kuhusika na mauaji ya raia 28 wa Kenya kwa madai ya kutokujua kusoma Koran Tukufu na kufanikiwa kukisambaratisha, na wanamgambo 100 kuwawa. Kikundi hiki cha Al Shabaab baada ya kuteka nyara Bus na kufanya mauaji ya kinyama kilikimbilia nchini Somalia.

Bwana William Ruto, Makamu wa Rais wa Kenya ameyasema hayo siku ya Jumapili tarehe 23 Novemba 2014 wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Nairobi na kuongeza kwamba, vikosi vya ulinzi na usalama vimesambaratisha pia kambi na baadhi ya magari yaliyokuwa yanatumiwa na wanamgambo hao katika vitendo vya kigaidi. Serikali ya Kenya imetangaza kwamba, kwa wale wote watakaosababisha mauaji ya raia wasiokuwa na hatia, watatafutwa ili haki iweze kutendeka.

Umoja wa Mataifa pamoja na nchi kadhaa zililaani mauaji ya wananchi 28 kutoka Kenya kwa misingi ya kidini, lakini kwa sasa changamoto kubwa ni kwa Serikali ya Kenya kuhakikisha kwamba, inatoa kipaumbele cha kwanza kwa ulinzi na usalama wa raia na mali zao, kwani hofu na wasi wasi vinazidi kujengeka kutoka na vitendo vya kigaidi nchini Kenya, hali ambayo inadhohofisha pia sekta ya utalii ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa pato ghafi la taifa!







All the contents on this site are copyrighted ©.