Watu 28 wauwawa kikatili nchini Kenya kwa vile hawakujua kusoma Koran Tukufu!
Serikali ya Kenya imewahakikishia wananchi wake kwamba, itawasaka kwa udi na uvumba
wale wote waliohusika na mauaji ya kinyama ya watu 28 ambao sio wa dini ya Kiislam
kwa vile walishindwa kusoma Koran, ili kuwafikisha kwenye mkondo wa sheria.
Ni
maneno mazito yaliyotolewa na Bwana Willim Ruto, Makamu wa Rais wa Kenya, wakati alipokuwa
anazungumza na wananchi wa Kenya kwa njia ya Televisheni baada ya Magaidi wanne wa
Kikundi cha Al Shabaab kuteka nyara Bus na hatimaye kufanya mauaji ya kinyama.
Kikundi
cha kigaidi cha Al Shabaab, Jumamosi, tarehe 22 Novemba 2014 kimejigamba kwa kusema
kwamba, wanamgambo wake wameteka Bus lililokuwa linasafiri karibu na mpaka wa Kenya,
Somalia na Ethiopia na kuwauwa "Kafiri" 28, kama kitendo cha kulipiza kisasi kutokana
na upekuzi uliofanywa na Jeshi la Polisi kwenye misikiti kadhaa inayoshukuwa kutumiwa
na vikundi vya kigaidi kuchafua amani na utulivu nchini Kenya.