2014-11-22 15:22:21

Kardinali Angelini, Baba na mfariji wa wagonjwa afariki dunia!


Kardinali Angelo Sodano, Dekano wa Makardinali, Jumatatu tarehe 24 Novemba 2014 majira ya saa 9:00 Alasiri, anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumwombea Marehemu Kardinali Fiorenzo Angelini, Rais mstaafu wa Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa wafanyakazi katika sekta afya, aliyefariki dunia tarehe 22 Novemba 2014 mjini Vatican akiwa na umri wa miaka 98. Mara baada ya Ibada ya Misa Takatifu, Baba Mtakatifu Francisko ataongoza Ibada ya Mazishi kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Baba Mtakatifu amemkumbuka kwa namna ya pekee wakati wa kufunga mkutano wa ishirini na tisa wa Baraza la Kipapa la huduma kwa wafanyakazi katika sekta ya afya, uliokuwa unafanyika mjini Vatican. Marehemu Kardinali Angelini alizaliwa kunako tarehe Mosi, Agosti 1916 mjini Roma, akapadrishwa kunako tarehe 3 Februari 1940 na katika maisha na utume wake kama Padre akajisadaka kwa ajili ya maskini na wagonjwa; akafundisha na kuwafunda vijana Wakatoliki Italia.

Kunako mwaka 1956 akateuliwa kuwa Askofu na kupewa dhamana ya kuwa ni msimamizi wa maisha ya kiroho kwa wagonjwa katika Kliniki na Hospitali za Roma. Tangu mwaka 1977 hadi mwaka 1985 alikuwa ni Askofu msaidizi wa Jimbo kuu la Roma. Tarehe 11 Februari 1985 akateuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Rais wa muda wa Tume ya Kipapa ya huduma za kichungaji kwa wafanyakazi katika sekta ya afya, tume ambayo kunako mwaka 1988 ikapandishwa hadhi na kuwa ni Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa wafanyakazi katika sekta ya afya.

Wakati wote wa maisha yake kama Padre, Askofu na Kardinali aliguswa sana na mahangaiko ya wagonjwa na maskini. Kunako mwaka 1959 alianzisha Chama cha Madaktari Wakatoliki nchini Italia, akasaidia kukoleza moyo wa huduma za kichungaji kwa wagonjwa mara baada ya maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, sanjari na mabadiliko ya Sakramenti ya Mpako wa mwisho, ukaanza kuitwa Mpako wa Wagonjwa, ili kuonja huruma, upendo na msamaha kutoka kwa Yesu mganga mkuu!

Ni kiongozi aliyejisadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wagonjwa: kiroho na kimwili, akasaidia kuandaa mikutano mikubwa ya kimataifa kwa ajili ya kutafakari kanuni maadili, utu na heshima ya binadamu katika sekta ya afya. Kunako tarehe 28 Juni 1991 akateuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Kardinali.







All the contents on this site are copyrighted ©.