2014-11-22 08:44:19

Kanisa bado lina mchango wa pekee katika ujenzi wa Jumuiya Ulaya


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anabainisha kwamba, Baba Mtakatifu Francisko hapo tarehe 25 Novemba 2014 anatarajiwa kufanya hija yake ya kikazi mjini Strasbourg, ili kuzungumza na wajumbe wa Bunge la Ulaya pamoja na Baraza la Ulaya, baada ya kupita takribani miaka 26 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipotembelea na kuzungumza na wajumbe wa taasisi hizi, huku akisisitizia umuhimu wa kushikamana kulinda na kutunza mazingira, kuwahudumia wahamiaji na wakimbizi pamoja na kuwa na mwono sahihi wa binadamu.

Kardinali Parolin anasema, haya ni mambo ambayo bado ni changamoto endelevu inayovaliwa njuga na Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba zake mbali mbali. Anasema, umoja na mshikamano ni tunu msingi zinazounganisha Nchi za Umoja wa Ulaya na kwamba, zinapaswa kuwa na mwelekeo sahihi juu ya binadamu na haki zake msingi pamoja na kukabiliana na changamoto zinazotaka kudhalilisha utu na heshima ya binadamu.

Taasisi za Ulaya hazina budi kutoa majibu sahihi kwa kero na changamoto zinazowakabili watu wake, jambo linalohitaji kuwekeza zaidi katika elimu na majiundo makini kwa vijana wa kizazi kipya, ili kuendeleza tunu msingi za maisha kama zilivyoasisiwa na waanzilishi wa Jumuiya ya Ulaya. Kuna vijana zaidi ya millioni 75 Barani Ulaya ambao hawana fursa za ajira wala nafasi ya kuweza kujiendeleza kutokana na ukata. Ni hali ambayo inatisha kwani umaskini wa hali na kipato unaendelea kuongezeka siku hadi siku Barani Ulaya; mambo yanayotishia: haki, amani na utulivu.

Umoja wa Ulaya unapata chimbuko lake kutoka katika tunu msingi za maisha ya Kikristo; changamoto ya kuendelea kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu, uhuru wa kweli, demokrasia, usawa na utawala wa sheria. Kanisa bado linadhamana ya kuchangia katika ustawi na maendeleo ya Bara la Ulaya kwa kujikita katika majadiliano ya kina kati ya imani na uwezo wa mwanadamu kufikiri na kutenda, dhamana iliyotiliwa mkazo sana na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI; ili kushirikiana na kushikamana kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi.

Baba Mtakatifu wakati wa ziara yake ya kikazi huko mjini Strasbourg atakutana na wabunge wa Ulaya pamoja na kuzungumza na Baraza la Ulaya linalounganisha mataifa 47; kila kundi linatarajiwa kupewa changamoto maalum na umuhimu wa kushikamana kwa pamoja, ili kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani pamoja na kuendeleza haki msingi za binadamu, kama vikolezo maalum vya ujenzi wa Bara la Ulaya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.