2014-11-22 14:34:29

Jifungeni kibwebwe ili kupata tiba na vifaa tiba kwa ajili ya kuzuia na kuponya ugonjwa wa mtindio wa ubongo!


Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa wafanyakazi katika sekta ya afya, Jumamosi tarehe 22 Novemba 2014 limehitimisha mkutano wake wa ishirini na tisa uliokuwa unajadili jinsi ya kuwahudumia wagonjwa wenye mtindio wa ubongo, ili kuwajengea tena matumaini.

Askofu mkuu Zygmunt Zimowski, anasema Baraza lake la Kipapa limeandaa mkutano huu, ili kukabiliana vyema zaidi na changamoto zinazoibuliwa katika ugonjwa huu. Kilele cha mkutano huu ni pale wadau walipokutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Ukumbi wa mikutano wa Paulo VI ulioko mjini Vatican.

Baba Mtakatifu katika hotuba yake, anawashukuru wadau mbali mbali kwa kupembua kwa kina na mapana tema hii ambayo inagusa wengi; tema ambayo imewapatia wajumbe fursa ya kusali na kusikiliza shuhuda mbali mbali zilizotolewa na wagonjwa, familia na vyama vya kitume, changamoto kubwa kwa Serikali, Wataalama na Kanisa katika ujumla wake kuhakikisha kwamba, wanawasaidia waathirika wa ugonjwa wa mtindio wa ubongo kwa kuthubutu kukutana nao, kuwakaribisha, kuwaonjesha upendo na mshikamano unaobubujika matumaini mapya, ili kuondokana na unyanyapaa wanaokumbana nao, mambo yanayochangia usumbufu mkubwa kwa wagonjwa na familia zao.

Kanisa linapenda kuwasindikiza wagonjwa hawa kwa kusikiliza kwa makini matatizo yanayotokana na ugonjwa wao, ili wagonjwa na familia zao, waweze kuipokea hali hii bila kuona aibu au kutumbukia kwenye upweke hasi. Ili kuwasaidia wagonjwa hawa kuna haja ya kujenga mtandao katika maeneo husika ili kutoa huduma makini inayowahusisha watu wengi zaidi na wala si wazazi peke yao, kwani kundi hili linaweza kuwaondolea mawazo na hali ya kuchanganyikiwa.

Baba Mtakatifu Francisko ametumia fursa hii kuwapongeza wadau mbali mbali wanaoendelea kutoa huduma ili kuwasaidia wagonjwa wenye mtindio wa ubongo na familia zao. Anaendelea kuwahimiza watalaam, mabingwa na watafiti kujifunga kibwebwe ili kuhakikisha kwamba, wanapata haraka iwezekanavyo tiba na vifaa tiba, ili kuponya, lakini zaidi kukinga watoto kutokana na ugonjwa huu. Yote haya yafanyike kwa kuzingatia haki msingi za mgonjwa, mahitaji yao msingi na nguvu walizonazo, daima utu na heshima ya binadamu vikipewa kipaumbele cha kwanza.

Baba Mtakatifu Francisko kwa namna ya pekee amemkumbuka na kumwombea Kardinali Fiorenzo Angelini, aliyefariki dunia mjini Roma akiwa na umri wa miaka 98. Kardinali Angelini ni muasisi wa Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa wafanyakazi katika sekta ya afya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.