2014-11-22 14:41:23

Iweni mashahidi wa upendo na huruma ya Mungu!


Simama nenda mjini Ninawi, Ukatangaze Injili, ndiyo kauli mbiu iliyoongoza maadhimisho ya Kongamano la Nne la Kitaifa lililoandaliwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, kama sehemu ya mchakato unaopania kuendeleza na kukuza ari na moyo wa kimissionari nchini Italia, ili kuwahamaisha waamini kushiriki kikamilifu katika azma ya Uinjilishaji mpya, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Kongamano hili limeadhimishwa miaka kumi baada ya Kongamano kama hili kufanyika huko Montesilvano; lakini kwa wakati huu wamejikita katika mambo makuu matatu yaani: Uhamasishaji, ushirikiano na majiundo, ili kukoleza ari na moyo wa kimissionari miongoni mwa waamini; kongamano ambalo limehudhuriwa na washiriki zaidi ya 700.

Baba Mtakatifu Francisko akizungumza na wajumbe hawa, Jumamosi, tarehe 22 Novemba 2014 amewakumbusha kisa cha Nabii Yona aliyeshikwa na woga kiasi cha kukataa kwenda Ninawi kutangaza Habari Njema ya Wokovu, lakini kutokana na huruma pamoja na upendo wa Mungu anafanikiwa kwenda mjini hapo na mambo kweli yanabadilika; waamini hawawezi kumtumikia Mungu na mali!

Huu ni mwaliko wa kuendeleza moyo wa kimissionari, bila ya kuogopa kukutana na watu pamoja na kugundua mambo mapya, ili kuwatangazia watu wote Injili ya Furaha na kwamba, utangazaji wa Habari Njema kwa watu wa Mataifa ndio utume wa Kanisa ulimwenguni, ili kutoka kwenda: kusikiliza kilio cha maskini pamoja na kukutana na wote, ili kuwatangazia Injili ya Furaha.

Familia ya Mungu nchini Italia haina budi kuendeleza moyo wa upendo na mshikamano katika kuwatangazia watu wa Mataifa Habari Njema ya Wokovu, kwani hii ni dhamana kwa Wakristo wote, ili kupata wongofu wa kimissionari kwa ajili ya Kanisa zima kwa kuwashirikisha wengine, kile kilichoko katika mioyo yao kama walivyofanya Mitume Andrea na Yohane baada ya kukutana na Yesu kwa mara ya kwanza.

Baba Mtakatifu analipongeza Kanisa Katoliki nchini Italia kwa kutoa Mapadre wengi wanaoendelea kujisadaka sehemu mbali mbali za dunia, ili kuwatangazia Watu wa Mataifa Injili ya Furaha, zawadi kubwa kwa Kanisa la Kiulimwengu, mwaliko wa kuendelea kuimarisha waamini katika matumaini, ili kuleta mabadiliko kwa kujikita katika mambo msingi yanayogusa maisha ya mwanadamu, kwani watu wengi wanasubiri kusikia neno la: huruma, faraja na matumaini, kwani Injili ya Kristo inamwilishwa katika historia na maisha ya watu.

Yesu alijitahidi kuwatafuta watu waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa Jamii; akajitahidi kukutana na kuwasaidia maskini, kuwaponya wagonjwa, kutoa pepo wachafu, kusamehe dhambi pamoja na kuunda kundi dogo la wafuasi waliomsikiliza na kumhudumia, huu ukawa ni mwanzo wa mabadiliko makubwa katika maisha ya kiroho na kiutu, kiini cha Habari Njema ya Wokovu kutoka kwa Yesu Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu kwa ajili ya watu wake.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini nchini Italia kukuza na kudumisha ari na moyo wa kimissionari katika maeneo yao, kwani watu wengi bado wana kiu na njaa ya kusikiliza Injili ya Furaha. Wamissionari ambao wamekuwa ni mashahidi wa imani na mapendo wanaonesha kwamba, ushindi unaweza kupatikana kwa njia ya silaha ya upendo, kwa kujisadaka kwa ajili ya Kristo na maskini wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Wakristo wanapaswa kutoka ili kuonja shida na mahangaiko ya watu kutokana na: umaskini, vita, kinzani za kijamii na uhalifu; bila kusahau wazee wanaotelekezwa, watoto wadogo na wote wanaohitaji msaada wao wa daima. Waamini wajitahidi kuwa kweli ni vyombo vya amani inayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ili kweli waweze kuwa ni mashahidi wa upendo na huruma yake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.