Wagonjwa wa mtindio wa ubongo, wahudumiwe ndani ya familia!
Mkutano wa ishirini na tisa wa Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa wafanyakazi
katika sekta ya afya, umefunguliwa rasmi tarehe 20 Novemba 2014, kwa Ibada ya Misa
Takatifu iliyoongozwa na Kardinali George Pell, Mwenyekiti wa Sekretarieti ya Kipapa
kwa ajili ya uchumi.
Wajumbe wanaendelea kukazia umuhimu wa kutafuta tiba
ya ugonjwa wa mtindio wa ubongo kuanzia ndani ya Familia, kwa kushirikiana na wataalam,
watafiti na mabingwa katika sekta ya afya, ili kuwajengea matumaini wagonjwa wa mtindio
wa ubongo ambao kwa sasa wanakadiriwa kuwa ni asilimia moja ya idadi yote ya watu
duniani. Ni ugonjwa unaoacha madhara makubwa kwa mgonjwa, familia na jamii katika
ujumla wake, ili kuwajengea matumaini pasi na kukata tamaa.
Wajumbe wamesikiliza
shuhuda mbali mbali zilizotolewa na wagonjwa pamoja na familia zao, jinsi ambavyo
wanajitahidi kuwahudumia kwa imani na mapendo; kwani familia ni mahali murua zaidi
katika kuwahudumia wagonjwa wenye mtindio wa ubongo. Bibi Beatrice Lorenzin, Waziri
wa Afya nchini Italia amewaambia wajumbe kwamba, idadi ya wagonjwa wa mtindio wa ubongo
inaongezeka maradufu Barani Ulaya na kwamba, kampeni dhidi ya ugonjwa huu inakwamishwa
na imani potofu kwamba, mtindio wa ubungo unasababishwa na chanjo zinazotolewa kwa
watoto wadogo.
Wataalam na mabingwa wa ugonjwa huu, wanakazia kwamba, kuna
haja ya kufanya utafiti wa kina kuhusu chanzo cha ugonjwa huu na umuhimu wa familia
kuwahudumia watu wenye ugonjwa huu, wakiwa ndani ya familia badala ya kuwatelekeza.
Lengo ni kufuatilia maendeleo ya mgonjwa, kwa uchunguzi na tiba zaidi. Mkutano huu
unafungwa rasmi, Jumamosi, tarehe 22 Novemba 2014 kwa kukutana na kusherehekea kwa
pamoja na Baba Mtakatifu Francisko.