Kanuni maadili inalenga kudumisha utu wa binadamu na mafao ya wengi!
Jimbo Kuu la Verona, Italia kuanzia tarehe 20 hadi tarehe 23 Novemba 2014 linaadhimisha
Tamasha la nne la Mafundisho Jamii ya Kanisa, linaloongozwa na kauli mbiu "Nje ya
mahali na ndani ya nyakati", changamoto ya kuhakikisha kwamba, Kanisa linasaidia kutibu
na kuganga madonda na machungu ya watu wasiokuwa na fursa za ajira, ili kuwarudishia
tena hadhi na utu wao kama binadamu. Tatizo kubwa linalojitokeza ni kufumbia macho
na masikio mahangaiko ya watu wasiokuwa na ajira.
Baba Mtakatifu Francisko
katika ujumbe wake kwa njia ya video katika kongamano hili anasema kwamba, kanuni
maadili inayofundishwa na Mama Kanisa inapania pamoja na mambo mengine, kutoa kipaumbele
cha kwanza kwa mafao ya wengi na huduma kwa jirani, ili kila mtu aweze kufurahia matunda
ya kazi ya uumbaji. Wafanyabiashara na wachumi, wanakumbushwa kwamba, fedha ni kwa
ajili ya kumhudumia mwanadamu na kamwe isiwe ni chanzo cha nguvu ya kiuchumi na nyanyaso
kwa maskini.
Baba Mtakatifu anasema kuna malalamiko mengi kwamba mipango mingi
ya maendeleo na utunzaji wa mazingira haiwezi kutekelezeka kutokana na ukata pamoja
na hali mbaya ya uchumi, lakini bado kuna kiasi kikubwa cha fedha kinachopatikana
kwa ajili ya kununulia silaha zinazoleta maafa na majanga katika maisha ya watu. Lakini
pesa peke yake haiwezi kuchochea maendeleo, bali mwanadamu anayeitumia fedha hii kwa
hekima na busara anaweza kuwa ni kikolezo kikuu cha maendeleo, kumbe kuna haja ya
kuwa na wajasiriamali wanaothubutu kuwekeza kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya jamii
zao.
Wajasiriamali wanapaswa kuwekeza katika teknolojia, lakini zaidi kwa kuboresha
mahusiano ya watu, ili watu wengi zaidi waweze kushiriki huku wakiongozwa na kanuni
ya mshikamano kati ya watu, ili kwa pamoja kuweza kutafuta suluhu ya matatizo na changamoto
zinazojitokeza, ili kuthamini utu wa watu na kuwawezesha kujitegemea wenyewe, ili
kuwa na matumaini ya kesho iliyo bora zaidi. Huu ni mchakato wa maendeleo unaojikita
katika upendo na mshikamano, ili kujibu changamoto za kijamii.
Baba Mtakatifu
anasema, kuna haja ya kufanya mabadiliko katika maisha, kwa kuwashirikisha wengine
ule upendo unaobubujika kutoka katika undani wa maisha ya mtu pamoja na kutumia karama
na vipaji alivyokirimiwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya mafao na ustawi wa wengi.
Hapa watu watumie akili, ujuzi, maarifa na uwezo kwa ajili ya wengi na kuondokana
na tabia ya uchoyo na wivu usiokuwa na mashiko; mambo yanayopelekea watu kutojiamini
na hatimaye kuanza kudhaniana vibaya. Umwilishaji wa karama ni chemchemi ya furaha
na matumaini makubwa miongoni mwa vijana.
Baba Mtakatifu Francisko anasema,
kuna idadi kubwa ya vijana ambao hawana fursa za ajira, mwaliko kwa wadau mbali mbali
kutumia muda waliopewa na Mwenyezi Mungu, ili kushirikishana hazina ambayo wamekabidhiwa
na Mungu, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi, ili kupata utimilifu wa maisha
ya binadamu. Baba Mtakatifu anawashukuru viongozi wa Jimbo Kuu la Verona kwa kujielekeza
zaidi katika kuunda dhamiri nyofu zinazoelewa changamoto za kijamii na ufumbuzi wake.