Jitokezeni kuchukua formu na kushiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa
Serikali ya Tanzania imesema kuwa itatumia jumla ya shilingi bilioni 20 kwa ajili
ya matumizi ya zoezi la uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Desemba
mwaka 2014 hadi kukamilika. Gharama hizo zimetolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Serikali
za Mitaa Ofisi ya Waziri Mkuu Tamisemi, Kharist Luanda, alipokuwa akizungumza na waandishi
wa habari ofisini kwake mjini Dodoma. Alisema kuwa gharama hizo zinajumuisha tangu
kuanza kwa zoezi mzima la maandalizi ya uchaguzi huo wa serikali za mitaa mpaka siku
ya upigaji wa kura utakapokamilika.
Alisema kuwa gharama zingine ambazo zitakazotumika
kwenye matumizi ya fedha hizo,ni pamoja fedha za kusafirisha masanduku,posho,usafiri,kulipa
wasimamizi wa uchaguzi huo na semina mbalimbali zilizokuwa zikitolewa kwa ajili ya
elimu. Akizungumza kuhusu zoezi la uandikishaji wa wapiga kura alisema kuwa bado watanzania
hawana mwitikio wa kujitokeza katika kujiandikisha na kuchukua fomu za kugombea, hivyo
amewataka kujitokeza ili waweze kutimiza haki yao ya kuwapata viongozi wanaokubarika.
Alisema
kwa kufanya hivyo wataepukana na kupiga makelele na tabia ya kuchaguliwa viongozi
kutokana na kutojitokeza ambako watanzania wengi wameshindwa kutumia haki yao hiyo.
Mkurugenzi
huyo aidha alifafanua kuwa uandikishaji wa wapiga kura wa mwaka huu wa 2014 katika
chaguzi zake za serikali za mitaa utafanyika kwa kutumia Daftari la wakazi badala
ya kutumia daftari ya kudumu ya wapiga kura inayotumika kwa viongozi wa ngazi ya udiwani,wabunge
hadi Rais.
Luanda alisema kuwa uandikishaji huo wa wapiga kura kwa mwaka huu
pia utafanyika kwenye majengo ya umma na pale ambapo itaonekana hakuna jengo la umma,basi
utafanyika katika sehemu ambayo wasimamizi wa uchaguzi watakubaliana na viongozi wa
vyama vya siasa. Hata hivyo Mkurugenzi huyo alisema kuwa zoezi la kuanza kuchukua
fomu za kugombea litaanza tarehe, 23-29 /11 mwaka huu,hivyo akawataka wale wote watakaogombea
kupitia vyama vyao vya siasa wafike kwenda kuchukua fomu kwa wasimamizi wa vituo.
“Ninaomba
wagombea watakapochukua fomu hizo wahakikishe wanasoma maelekezo kwa makini, ili kuepuka
kuwekewa pingamizi na wagombea wengine kwa madai kukiuka ujazaji wa fomu hizo vibaya”alisema.
Mkurugenzi huyo kuhusu nembo zitakazotumika kwenye fomu ya kugombea kwenye chaguzi
hizo, alisema kuwa kila fomu itakuwa na nembo ya Halmashauri husika na nembo ya chama
cha siasa chenye wagombea.