Jumuiya ya Kimataifa inaendelea kujipanga vyema ili kuweka bayana mikakati ya maendeleo
endelevu itakayofanyiwa kazi mara baada ya kukamilika kwa Malengo ya Mendeleo ya Millenia
hapo mwaka 2015, kwa kujikita zaidi katika mchakato wa mapambano dhidi ya umaskini
wa kutupwa; kwa kulinda na kutunza mazingira.
Hizi ni changamoto kubwa ambazo
Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kupambana nazo, ili kudhibiti madhara yanayosababishwa
na mabadiliko ya tabianchi ambayo yanaendelea kutishia usalama wa maisha ya watu na
mali zao sehemu mbali mbali za dunia. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuanza kutekeleza
malengo yake ili kudhibiti hewa ya ukaa inayozalishwa kwa wingi kutokana na teknolojia
isiyokuwa rafiki kwa mazingira.
Akichangia hoja kwenye mkutano mkuu wa Baraza
la Umoja wa Mataifa uliokuwa unajadili kuhusu mikakati ya maendeleo endelevu na utunzaji
bora wa mazingira, Askofu mkuu Benedito Auza, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye
Umoja wa Mataifa anasema kwamba, utunzaji bora wa mazingira ni sehemu muhimu sana
ya uwajibikaji wa kimaadili na haki. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujiandaa kikamilifu
katika mkutano wa tabianchi unaotarajiwa kufanyika mjini Paris, Ufaransa, Desemba
2015.
Jumuiya ya Kimataifa itambue kwamba, watu wote wanategemeana, hata matajiri
wanawategemea maskini na kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inaweza kupata mafanikio makubwa,
ikiwa kama watashikamana kwa pamoja kutekeleza Itifaki ya mwaka 2020 inayopania kupunguza
hewa ya ukaa kwa kiasi kikubwa, kwa kutambua kwamba, watu wanawajibika kutunza mazingira
kama sehemu ya haki msingi za binadamu. Utunzaji wa mazingira uwe ni kwa ajili ya
mafao ya wengi na wala si kwa ajili ya watu wachache katika jamii, changamoto ya kubadili
mtindo wa maisha kwa kuwajibika zaidi.
Askofu mkuu Auza anasema, dunia kwa
sasa inaonekana kuwa kama kijiji, kumbe, kuna haja ya kuwa na uwajibikaji wa pamoja,
dhamana inayopaswa kutekelezwa na Serikali pamoja na watunga sera, ili watu waweze
kuishi katika mazingira bora kwa sasa na kesho yenye matumaini makubwa zaidi. Utunzaji
bora wa mazingira unahitaji sera na mikakati makini ya kiuchumi inayopangwa na kutekelezwa
na Jumuiya ya Kimataifa, kwa kuzingatia kanuni msingi za kimaadili na kisayansi.