Baa la njaa ni matokeo ya ukosefu wa sera makini katika mikakati ya uzalishaji, ugavi
na masoko; ni kielelezo cha ubinafsi unaowafanya baadhi ya watu kufaidika zaidi kwa
kula na kusaza na hata pengine kumwaga chakula hiki, wakati kuna maelfu ya watu wanakufa
kwa baa la njaa sehemu mbali mbali duniani. Kuna haja ya kuwa na sera makini katika
sekta ya kilimo ili kuwa na uhakika wa usalama wa chakula kinachokidhi viwango vya
kimataifa ili kukabiliana pia na lishe duni.
Katika mahojiano
maalum na Radio Vatican, Dr. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania ambaye anaongoza ujumbe wa Tanzania katika mkutano wa kimataifa kuhusu
lishe ulioandaliwa na Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa anasema kwamba,
Sera ya Kilimo kwanza inaendelea kupata mafanikio makubwa nchini Tanzania kutokana
na ongezeko la uzalishaji wa mazao ya chakula kiasi kwamba kwa sasa Tanzania ina ziada
ya chakula kwa asilimia 20%.
Sera ya Kilimo kwanza imepata mwitikio mkubwa
kwani watanzania wengi kwa sasa wanatumia pembejeo za kisasa katika uzalishaji, kiasi
kwamba, Serikali inaanza kujipanga ili kujenga maghala makubwa kwa ajili ya kuhifadhi
nafaka zinazozalishwa na wakulima sehemu mbali mbali za nchi.
Serikali inaendelea
kuboresha mfumo wa masoko, ili wakulima waweze kuwa na uhakika wa soko la mazao wanayoyazalisha,
kwa kuwa na mfumo wa kubadilishana mazao sokoni. Zoezi hili limepata mafanikio makubwa
nchini Ethiopia na Serikali ya Tanzania inasema, inataka kuona mafanikio haya pia
kwa wakulima wake. Dr. Bilal anasema, mafanikio ya Sera ya Kilimo kwanza ni kutaka
kuharakisha ustawi na maendeleo ya wakulima wengi nchini Tanzania kwa kuwa na uhakika
wa chakula.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio
Vatican.