Injili ya Uhai ni matunda ya mkamilishano kati ya Bwana na Bibi!
Mkamilishano kati ya Bwana na Bibi, daima limekuwa ni jambo ambalo linavuta hisia
za watu wengi, kiasi hata cha kuwaacha watu wakiwa wamshikwa na bumbuwazi. Huu ni
mkamilishano usiofungwa na mambo ya fedha na biashara, bali katika upendo unaobubujika
kutoka katika undani wa mtu.
Haya ndiyo yaliyojiri katika kongamano la kimataifa
la majadiliano ya kidini lililoandaliwa na Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya
Kanisa kwa kushirikiana na Mabaraza mengine ya Kipapa ili viongozi wa kidini kuweza
kujadili mkamilishano kati ya Bwana na Bibi, tangu tarehe 17 hadi tarehe 19 Novemba
2014 hapa mjini Vatican. Itakumbukwa kwamba, kongamano hili lilifunguliwa na Baba
Mtakatifu aliyekazia umuhimu wa watoto kupata wazazi wote wawili, yaani Baba na Mama
na wala si vinginevyo.
Kongamano hili limewashikirisha viongozi mbali mbali
wa kidini, ambao kwa pamoja wamekiri ukuu na umuhimu wa maisha ya ndoa na familia
kadiri ya mpango wa Mungu. Bwana na Bibi kwa hiyari yao wenyewe wanaamua kufungamana
katika maisha; katika raha na shida; katika afya na magonjwa, wakipendana na kuheshimiana
siku zote za maisha yao. Mkamilishano huu ni chemchemi ya maisha mapya na mwendelezo
wa jamii ya binadamu.
Wajumbe wa kongamano la mkamilishano kati ya Bwana na
Bibi wanatambua mchango mkubwa unaoweza kutolewa na ndugu, jamaa na marafiki kwa wanandoa
wapya katika hija ya maisha yao ya kila siku, kwa njia ya mifano bora ya maisha na
ushauri mwanana, lengo likiwa na kudumisha maisha ya ndoa na familia. Hili ni kundi
ambalo linakuwa la kwanza kufaidika na ndoa dumifu, kwani wamewekeza kwa dhati katika
ustawi na maendeleo ya wanandoa wenyewe.
Muungano kati ya Bwana na Bibi unapania
kuendeleza Injili ya Uhai kwa binadamu na tamaduni zake, lakini ni taasisi inayokabiliwa
na changamoto nyingi na tete. Ndoa za uhakika zisizofungamana na "mshiko" zinaendelea
kupungua na kwamba, upendo umegeuzwa kuwa bidhaa na chombo cha kampeni inayokumbatia
utamaduni wa kifo. Ndoa ni mahali ambapo, binadamu anawekeza kwa ajili ya Injili ya
Uhai!