2014-11-19 11:54:43

Onesho la maisha, maneno na picha za Mtakatifu Francisko wa Assis, Umoja wa Mataifa!


Askofu mkuu Bernadito Auza, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa, Jumatatu tarehe 17 Novemba 2014 amefungua maonesho ya Mtakatifu Francisko wa Assis kuhusu: historia fupi ya maisha yake, maneno muhimu aliyosema na baadhi ya picha zilizochorwa kama kumbu kumbu ya maisha yaliyogusa watu wengi, kiasi cha kufanya maamuzi machungu! Onesho hili limefunguliwa kwenye Makao makuu ya Umoja wa Mataifa yaliyoko New York, Marekani, Nyumba ya Familia ya binadamu.

Askofu mkuu Auza anasema, nyaraka hizi ni muhimu na a ghali sana, kwani zinakumbusha umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika mchakato wa kutafuta, kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi; kwa kukuza umoja, udugu na mshikamano; ili kuondokana na kinzani, ukosefu wa haki, utumwa, nyanyaso na uharibifu wa mazingira.

Askofu mkuu Auza anasema, Baba Mtakatifu aliamua kuchukua jina la Mtakatifu Francisko ili kuonesha mshikamano wa pekee na maskini pamoja na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii; kusimama kidete kulinda na kutetea misingi ya haki na amani pamoja na kukazia umuhimu wa utunzaji bora wa mazngira.

Baba Mtakatifu Francisko anatarajia kutembelea Jimbo kuu la Philadelphia Marekani, Mwezi Septemba, 2015, habari ambayo imepokelewa kwa mikono miwili na waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema nchini Marekani.







All the contents on this site are copyrighted ©.