Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Jumapili iliyopita amehitimisha
ziara ya kikazi nchini Czech, kwa mwaliko wa Kardinali Dominik Duka, kama sehemu ya
maadhimisho ya Jubilee ya miaka 25 tangu Agnese wa Bohemia, alipotangazwa kuwa Mtakatifu,
kwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa la Mtakatifu Yohane Paulo II,
aliyemtangaza Agnese kuwa mtakatifu hapo tarehe 12 Novemba 1989.
Kardinali
Parolin, wakati wa mahubiri yake amemtaja Mtakatifu Agnese kuwa ni mtu anayependwa
na kuthaminiwa na waamini wengi, kwani kutangazwa kwake kuwa Mtakatifu kilikuwa ni
kiashilia cha kuanguka kwa utawala wa Kikomunisti nchini Czech na hapo ukawa ni mwanzo
wa mchakato wa demokrasia ya kweli na ujenzi wa umoja na mshikamano wa kitaifa. Jubilee
ya Mtakatifu Agnese imekwenda sanjari na kumbu kumbu ya miaka ishirini na mitano ya
kuanguka kwa utawala wa Kikomunisti.
Mtakatifu Agnese alikuwa na upendo mkubwa
kwa maskini na wote waliokuwa wanateseka kwa magonjwa na umaskini, mwaliko kwa waamini
kukesha na kuhakikisha kwamba, wanatumia vyema karama zao kwa ajili ya ustawi na maendeleo
ya Kanisa na Jamii inayowazunguka, kwa kutambua kwamba, kila mtu anawajibika kukuza
na kuendeleza karama ili ziweze kuzaa matunda yanayokusudiwa.
Waamini wamepewa
karama hizi kwa ajili ya mafao ya wengi na wala si kwa ajili ya matumizi ya mtu binafsi
peke yake. Kardinali Parolin amewataka waamini kutumia karama na vipaji vyao kwa ajili
ya kushikamana na wale wote wanaosimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya
binadamu, kwani Kristo anahamasishwa kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko, kutoka
na kuwaendea wengine ili kuwashirikisha Injili ya Furaha na Matumaini.