2014-11-19 14:17:35

Fanyeni maamuzi magumu ili kujenga upatanisho na amani!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 19 Novemba 2014 ameonesha masikitiko yake kutokana na kinzani za kidini na kijamii zinazoendelea kujitokeza katika Nchi Takatifu, kwa matukio ya mauaji ambayo yamepelekea walimu wanne wa dini ya Kiyahudi kupoteza maisha.

Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikishia wale wote walioguswa na matukio haya ya kinyama uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala. Kutoka katika undani wa moyo wake, anapenda kuwaalika wote wanaohusika kuachana na vitendo hivi vinavyosababisha mauaji ya watu wasiokuwa na hatia, kwa kufanya maamuzi magumu yanayojikita katika upatanisho na amani. Kujenga misingi ya amani ni kazi kubwa, lakini kuishi kwa amani, kweli yataka moyo!

Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kwamba hapo tarehe 21 Novemba, Kanisa litaadhimisha Siku kuu ya Bikira Maria kutolewa Hekaluni, sanjari na Siku ya Watawa wa Ndani, inayojulikana kwa lugha ya Kilatini, "Pro Orantibus".

Baba Mtakatifu anasema, hii ni fursa makini kwa Mama Kanisa kuwakumbuka na kuwaombea watawa wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya Mungu na jirani, katika sala na ukimya mtakatifu, huku wakitambua na kuthamini ukuu wa Mungu anayepaswa kupendwa na kuheshimiwa na wote. Ni wakati wa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa shuhuda zinazotolewa kwa njia ya maisha ya Watawa wa ndani, mwaliko wa kuhakikisha kwamba, wanapata mahitaji yao msingi: kiroho na kimwili, ili waendelee kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa Kristo na Kanisa lake.







All the contents on this site are copyrighted ©.