2014-11-18 11:58:03

Zakayo mtoza ushuru ni kielelezo cha toba na wongofu wa ndani!


Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Jumanne, tarehe 18 Novemba 2014 amewataka waamini kuchunguza dhamiri zao na kuona ikiwa kama kweli wanasikiliza sauti ya Roho Mtakatifu inayozungumza nao kutoka katika dhamiri nyofu, ili waweze kusonga mbele kwa kushuhudia imani inayomwilishwa katika matendo.

Dhamiri nyofu iwe ni dira na mwongozo wa maisha yao katika: Familia, Jamii na Kanisa kwa ujumla, bila ya kujikweza na kuwadharau wengine. Baba Mtakatifu ameonya tabia ya baadhi ya Wakristo kutaka kujikweza na kuwabeza wengine, wanaoonekana kuwa ni wadhambi na watu wasiokuwa na faida! Dhamiri nyofu, iwasukume Wakristo kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu, ili kweli waweze kushuhudia imani yao katika matendo.

Baba Mtakatifu amefanya rejea kwa Injili inayomwonesha Zakayo mtoza ushuru aliyetamani kumwona Yesu na alipokutana na Yesu, akaanza ukursa mpya wa maisha, akatubu na mkumwongokea Mwenyezi Mungu. Ni kiongozi aliyejinufaisha mwenyewe badala ya kuwahudumia wananchi, hali ambayo inaendelea hata leo hii, kiasi hata cha kuchukiwa na watu.

Zakayo alikuwa ni fisadi wa wakati wake, lakini aliweza kubadili maisha yake, kwa kutubu na kumwongokea Mungu baada ya kukutana na Yesu katika hija ya maisha yake. Hakuona kwamba, cheo chake kilikuwa ni jambo la kung'angania sana, bali akajitaabisha kwa kupanda mti ili kumwona Yesu aliyekuwa anasikia sana habari zake.

Zakayo ni kielelezo makini cha mwamini anayetubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu baada ya kuchunguza dhamiri yake kwa kina na mapana, kiasi cha kuwaacha wabaya wake wakinong'onezana kwamba, Yesu alikuwa ameingia na kula nyumbani kwa mdhambi! Uwepo wa Yesu katika nyumba ya Zakayo, uliweza kuitakatifuza na kumwezesha kuanza maisha mapya yanayosimikwa katika neema ya utakaso!







All the contents on this site are copyrighted ©.