2014-11-18 08:31:08

Hija ya kichungaji huko Strausbourg na Uturuki ni za kihistoria!


Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kutembelea Makao makuu ya Umoja wa Ulaya huko Strausbourg hapo tarehe 25 Novemba 2014, hii ikiwa ni hija yake ya tano kimataifa na tarehe 28 hadi 30 Novemba 2014 atafanya hija ya kiekumene nchini Uturuki; matukio ambao yana umuhimu wa pekee anasema Padre Federico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican wakati alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari mjini Vatican Jumatatu tarehe 17 Novemba 2014.

Ni kwa mara ya kwanza matukio haya yanafanyika katika kipindi kifupi kutokana na kalenda ilivyokaa kwa ajili ya Wabunge wa Bunge la Ulaya na Maadhimisho ya Siku kuu ya Mtakatifu Andrea, inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 30 Novemba. Patriaki Bartolomeo wa kwanza amemwalika Baba Mtakatifu Francisko kushiriki katika maadhimisho ya Siku kuu ya Mtakatifu Andrea kwa mwaka huu, ili kuendeleza hija ya kiekumene, iliyoanzishwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Padre Lombardi anasema, hija ya Baba Mtakatifu mjini Strausburg itakuwa ni fupi sana kuwahi kufanywa na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ni hija itakayodumu muda wa masaa manne tu, ambayo Baba Mtakatifu Francisko atapata nafasi ya kuhutubia Bunge la Ulaya pamoja na kuhutubia pia Baraza la Ulaya. Hii ni safari ya kikazi na wala haina uhusiano wowote na masuala ya kidini au maisha ya kiroho. Baba Mtakatifu anakwenda kuhutubia huko kwani Jumuiya ya Kimataifa inatambua dhamana na utume wake wa kimaadili na ndiyo maana vyombo hivi vina mahusiano ya kidiplomasia na Vatican.

Akiwa mjini Strausburg, Baba Mtakatifu atapata fursa ya kuzungumza na viongozi wa ngazi ya juu wa taasisi hizi za kimataifa kwa kugusia: matatizo, wajibu na changamoto zinazolikabili Bara la Ulaya. Kwa mara ya mwisho, Mtakatifu Yohane Paulo II alihutubia taasisi hizi kunako mwaka 1988, wakati huo bado Ukuta wa Berlin, kielelezo cha siasa za chuki na uhasama ukiwa bado umesimama.

Padre Lombardi anasema, hija ya kiekumene ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Uturuki ni mwendelezo wa hija ambazo zimewahi kufanywa na Mababa Watakatifu kama vile: Yohane XXIII, Paulo VI, Yohane Paulo II na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI. Baba Mtakatifu Francisko atakapowasili nchini Uturuki atakutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali na Wanadiplomasia.

Jumamosi, tarehe 29 Novemba, 2014, itakuwa ni siku maalum kwa ajili ya majadiliano ya kiekumene na udugu kati ya Wakristo na Waislam. Baba Mtakatifu atatembelea Makumbusho ya Sofia yanayofumbata mahusiano kati ya dini ya Kiislam na Kikristo. Atatembelea Msikiti mkuu wa Instanbul na baadaye Baba Mtakatifu atakutana na wawakilishi wa Jumuiya za Kikristo na baadaye jioni ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Roho Mtakatifu.

Jumapili, tarehe 30 Novemba 2014 baada ya kusalimiana na Rabi mkuu wa Uturuki, Baba Mtakatifu atashiriki katika Ibada Takatifu ya Kiekumene kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu George, kama sehemu ya maadhimisho ya Siku kuu ya Mtakatifu Andrea. Katika tukio, viongozi hawa wawili watatoa tamko la pamoja kuhusiana na mchakato wa majadiliano ya kiekumene.







All the contents on this site are copyrighted ©.