2014-11-18 09:06:30

Hakuna Kanisa pasi na huduma ya upendo!


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Jumamosi tarehe 15 Novemba 2014 akiwa mjini Prague, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Vito, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Jubilee ya Miaka 25 tangu Agnese wa Bohemia alipotangazwa kuwa Mtakatifu; mwanamke wa shoka aliyethubutu kuuza mali yake yote, ili kuwasaidia maskini na wote waliokuwa wanateseka kutokana magonjwa, kwa kuwajengea Hospitali na Monasteri ya Watawa ambao wangetoa huduma kwa maskini.

Kardinali Parolin katika mahubiri yake anasema kwamba, Mtakatifu Agnese ameacha urithi mkubwa wa maisha ya kiroho, kwa kuonesha upendo mkalimifu kwa Kristo na Kanisa lake kwa njia ya huduma makini kwa maskini na wagonjwa. Hii ni historia ya ushuhuda wa upendo inayofumbatwa katika maisha ya wananchi wa Jamhuri ya Czech kwa kutambua kwamba, upendo ni utambulisho muhimu wa Kanisa, pasi na upendo hakuna Kanisa, kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko.

Jubilee ya Miaka 25 tangu atangazwe kuwa Mtakatifu ni fursa kwa Kanisa kupembua kwa kina na mapana utakatifu wa maisha, ili kusonga mbele kwa imani na matumaini, kwa kujikita katika: uhuru wa kuabudu, demokrasia sanjari na kukazia utu na heshima ya binadamu, mambo msingi wakati huu Jamhuri ya Wananchi wa Czech wanapofanya pia kumbu kumbu ya Miaka 25 tangu Utawala wa Kikomunisti, ulipoangushwa na demokrasia ya kweli ikaanza kushika mkondo wake.

Kardinali Parolin alipkutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Czech, amegusia pia mateso, mahangaiko na madhulumu ambayo wananchi walikumbana nayo wakati wa Utawala wa Kikomunisti, kwa kipindi cha miaka arobaini, lakini bado kuna mashuhuda wa imani waliweza kujitokeza na kuonesha imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Anawapongeza Maaskofu wote waliopaaza sauti zao kwa ajili ya kupinga nyanyaso na dhuluma za kidini.

Kwa njia ya shuhuda makini za imani zilizotolewa na Familia ya Mungu, leo hii, Kanisa linafurahia matunda ya uhuru wa kuabudu pamoja na kushiriki kikamilifu katika mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu: kiroho na kimwili, mwaliko wa kujikita katika Uinjilishaji mpya ili kukabiliana na ukanamungu pamoja na mawazo mepesi mepesi.

Kardinali Parolin anasema, viongozi wa Kanisa wawasaidie waamini kutambua mizizi ya imani, ili kuimwilisha katika mchakato wa kuleta mabadiliko katika maisha ya watu, kwa kujenga na kuimarisha maadili na utu wema; upendo na mshikamano wa kitaifa; haki, amani na maendeleo kwa wote.







All the contents on this site are copyrighted ©.