2014-11-18 09:41:43

Bila familia, ubinadamu uko mashakani!


Familia inayoundwa na Bwana na Bibi ni msingi wa maisha ya kijamii unaotambulika na waamini wa dini mbali mbali duniani. Hii ni jumuiya ya kwanza ambamo mwanaume na mwanamke, wanaalikwa kujisadaka katika upendo wa dhati, ili kushiriki kikamilifu katika kazi ya uumbaji, dhamana ambayo mwanadamu amekabidhiwa na Mwenyezi Mungu.

Ni salam kutoka kwa Kardinali Gerhard Muller, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, wakati alipokuwa anamkaribisha Baba Mtakatifu Francisko kuzungumza na wajumbe 400 kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaowakilisha madhehebu na dini 14 duniani. Wajumbe hawa wanashiriki katika kongamano la kimataifa linalojadili kuhusu "mkamilishano kati ya mwanaume na mwanamke", Kongamano ambalo limefunguliwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 17 Novemba 2014 kwa kukazia umuhimu wa watoto kuwa na Baba na Mama watakaowaundia mazingira ya upendo, malezi na makuzi sahihi.

Kardinali Muller anasema, watu wasikubali kudanganywa na sera potofu kuhusu maisha ya ndoa na familia kwani bila familia, maisha ya mwanadamu yako hatarini. Kongamano hili limeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Baraza la Kipapa la Familia, Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini, Baraza la Kipapa linalohamasisha Umoja wa Wakristo pamoja na Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa.

Baba na Mama ni muhimu sana kwani wanawapatia watoto utambulisho, mapendo, matumaini na utu wao kama binadamu na kwamba, ni katika familia watu wanaanza kujifunza kujenga na kudumisha mahusiano na watu wengine. Upendo kati ya Bwana na Bibi katika maisha ya ndoa ni chanzo cha Injili ya Uhai, dhamana ambayo mwanadamu amepewa na Mwenyezi Mungu ili kuiendeleza.

Hawa wawili wakiungana kwa pamoja wanakuwa ni wazazi wenye dhamana na wajibu mbele ya Mungu na jamii. Hii ni sheria maumbile ambayo kamwe haiwezi kubalishwa na sera zinazokumbatia utamaduni wa kifo. Jamii itambue kwamba, mapendo ya kweli kadiri ya Mwenyezi Mungu yanasimikwa katika mahusiano kati ya Bwana na Bibi na wala si vinginevyo.







All the contents on this site are copyrighted ©.