2014-11-17 11:12:27

Papa amtembelea Kardinali Jorge Maria Mejia aliyelazwa hospitalini!


Baba Mtakatifu Francisko mara tu baada ya tafakari ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 16 Novemba 2014 aliondoka mjini Vatican kuelekea Castel Gandolfo, nje kidogo ya Roma, ili kuzindua sanamu ya chuma iliyotengenezwa na Msanii maarufu kutoka Argentina, Bwana Alejandro Marmo.

Katika safari, Baba Mtakatifu aliambatana na viongozi kadhaa kutoka Vatican, akabahatika kukutana na kuzungumza kwa kitambo kidogo na kikundi cha wananchi kutoka Argentina wanaofahamiana naye waliokuwa mjini Castel Gandolfo. Baadaye Baba Mtakatifu aliendelea na shughuli ya kubariki sanamu hizo.

Baadaye jioni wakati alipokuwa anarejea mjini Vatican, Baba Mtakatifu alikwenda kumtembelea Kardinali Jorge Maria Mejia, aliyelazwa kwenye Kliniki ya Pio wa Kumi na moja. Aliporejea mjini Vatican alikwenda moja kwa moja kusalimiana na vijana wanaoshiriki katika kongamano la kimataifa katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu na baadaye akarejea kwenye Makao yake yaliyoko kwenye Hosteli ya Mtakatifu Martha, mjini Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.