2014-11-17 08:48:02

Msifungie talanta zenu masandukuni, zitumieni kwa mafao ya wengi!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa tafakari kwa Sala ya Malaika wa Bwana, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 16 Novemba 2014 amekumbusha kwamba, Mwenyezi Mungu amemkirimia kila mwanadamu karama na mapaji maalum ambayo anapaswa kuyatumia kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi na wala karama hizi hazipaswi kufungiwa masandukuni.

Baba Mtakatifu anasema, Mwenyezi Mungu amewakirimia waamini karama ya: Neno. Ekaristi Takatifu, Imani, Upendo na Msamaha, mambo muhimu katika maisha ya mwamini, ambayo anapaswa kuyatumia ili yaweze kuzaa matunda yanayokusudiwa. Waamini wanapaswa kuondokana na woga usiokuwa na mashiko kwa kuhakikisha kwamba, karama zao zinazaa matunda kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi.

Huruma, wema na msamaha ni mambo ambayo Yesu mwenyewe anawakirimia wafuasi wake, ili waweze kuyatumia kwa ajili ya jirani zao, katika mazingira na medani mbali mbali za maisha; jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, Wakristo wanatolea ushuhuda wenye mashiko kuhusiana na imani yao, katika ukweli na uwazi.

Baba Mtakatifu anasema, Neno la Mungu linawahamasisha waamini kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake na kamwe wasizike Injili, bali wahakikishe kwamba, wanaitangaza kwa njia ya ushuhuda unaojikita katika uhalisia wa maisha. Hii ni nguvu inayoweza kumweka mtu katika mahangaiko, lakini inasafisha na kupyaisha maisha ya mwamini.

Baba Mtakatifu anakazia kwa namna ya pekee kabisa umuhimu wa waamini kujikita katika Msamaha unaotolewa na Kristo kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho. Sakramenti hii ni muhimu sana kwani inawasaidia waamini kuvunjilia mbali kuta za ubinafsi zinazopelekea mahusiano tenge, ili kuanza mchakato wa majadiliano, ambayo yatasaidia kukuza na kudumisha mawasiliano kati ya watu. Mwenyezi Mungu anatambua uwezo wa kila mtu na hivyo kumkirimia kadiri ya nafasi na haki ya Mungu.

Mwenyezi Mungu ana matumaini na wajawake, kamwe waamini wasimkatishe tamaa, wala kumdanganya kwa woga usiokuwa na mashiko, bali kulipa matumaini yanayoonesha matumaini ya kweli.

Baba Mtakatifu anasema, Bikira Maria alibahatika kupata zawadi kubwa na nzuri kuliko zote, yaani Yesu, Mwana wa Mungu; akamkirimia ubinadamu kwa kumwonjesha moyo wenye ukarimu na mapendo. Basi waamini wamwombe Bikira Maria ili aweze kuwajalia kuwa kweli ni watumishi wema na waaminifu, ili waweze kushiriki kikamilifu katika furaha ya Bwana wao.

Baba Mtakatifu Francisko, mwishoni amewataka waamini kusoma mfano wa talanta katika Injili kama ilivyoandikwa na Mathayo: 25:14- 30. Kila mwamini achunguze dhamiri yake ili kuona kama kweli zawadi alizokirimiwa na Mwenyezi Mungu, zinatumika kwa ajili ya mafao ya wengi au zinabinafishwa kwa ajili ya mafao ya mtu binafsi?

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.