Jitokezeni kwa wingi kuzungumzia mustakabali wa Tanzania kwa kukutana na Makamu wa
Rais
Dr. James Msekela Balozi wa Tanzania nchini Italia, Jumapili tarehe 16 Novemba 2014
alipata nafasi ya kuzungumza na Jumuiya ya Wanafunzi Watanzania Wakatoliki pamoja
na Watanzania wanaoishi mjini Roma, baada ya kuhudhuria Ibada ya Misa Takatifu kwa
ajili ya kuombea amani, ustawi na maendeleo nchini Tanzania.
Dr. Msekela
amewaambia watanzania kwamba, Dr. Mohamed Gharib Bilal anatarajiwa kuzungumza na watanzania
wanaoishi nchini Italia siku ya tarehe 18 Novemba 2014 kwenye Ukumbi wa Hotel ya Ambasciatori
Palace, iliyoko kwenye mtaa wa Vittorio Veneto namba 62, majira ya saa 9:00 Alasiri.
Makamu wa Rais atakuwa mjini Roma ili kuhudhuria mkutano wa pili wa lishe kimataifa
ambao umeandaliwa na Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa, FAO kwa kushirikiana
na Shirika la Afya Duniani, WHO, ili kuweka mikakati ya kupambana na baa la njaa pamoja
na lishe duni duniani.
Dr. Msekela anasema, awali, FAO ilikuwa imemwalika
Rais Jakaya Kikwete, lakini kutokana na sababu zisizozuilika hakuweza kuhudhuria katika
mkutano huu muhimu wa Kimataifa na badala yake, FAO imeendelea kuheshimu maamuzi yake
na hivyo Makamu wa Rais Dr. Mohamed Gharib Bilal anamwakilisha Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
Mkutano huu wa Lishe Kimataifa unafanyika tena baada
ya kupita takribani miaka 22 iliyopita. Watanzania wanaoishi nchini Italia watapata
nafasi ya kumsikiliza na kuzungumza na Makamu wa Rais kuhusiana na masuala mbali mbali
yanayohusu ustawi na maendeleo ya watanzania wote, hasa wakati huu Tanzania inapojiandaa
kukabiliana na changamoto ngumu kuhusiana na: chaguzi za Serikali za mitaa, Kura ya
maoni na uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika kunako mwaka 2015.
Dr. Msekela
ameipongeza pia Radio Vatican kwa kusaidia kuwahamasisha watanzania kuhudhuria tukio
hili kwa njia ya tovuti na matangazo yake. Ni matumaini ya Balozi wa Tanzania nchini
Italia kwamba, licha ya shughuli nyingi walizonazo watanzania, lakini walau wataweza
kutenga muda ili kuweza kukutana na Makamu wa Rais kwa ajili ya mustakabli wa Tanzania.