Balozi Mehmet Paçaci kutoka Uturuki awasilisha hati za utambulisho mjini Vatican
Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 17 Novemba 2014 amepokea hati za utambulisho
kutoka kwa Bwana Mehmet Paçaci, Balozi mpya wa Uturuki mjini Vatican. Hili ni tukio
muhimu sana la kihistoria wakati huu Baba Mtakatifu anapojiandaa kufanya hija ya kiekumene
nchini Uturuki.
Balozi Paçaci alizaliwa kunako tarehe 11 Septemba 1959 ameoa
na ana watoto watatu. Baada ya masomo yake kwenye Chuo Kikuu cha Ankara kunako mwaka
1989 akatunukiwa Shahada ya Uzamili katika masomo ya kitaalimungu. Alifaulu kuendelea
kufundisha Chuoni hapo kuanzia mwaka 1992 hadi mwaka 2008. Amewahi kuwa ni mshauri
katika masuala ya kidini na huduma za kijamii, katika Ubalozi wa Uturuki, mjini Washington
DC.
Kuanzia mwaka 2011 alikuwa ni mkurugenzi mkuu wa mambo ya nchi za nje
na ushirikiano wa kimataifa katika Ofisi ya rais inayoshughulikia masuala ya kidini.
Ni mtaalam wa lugha ya Kiarabu na Kiingereza.