2014-11-15 14:53:15

Uhuru na demokrasia ni mambo msingi katika ustawi na maendeleo ya binadamu!


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Ijumaa tarehe 14 Novemba 2014 amekutana na kuzungumza na Rais Milos Zeman wa Jamhuri ya Watu wa Czech; tukio ambalo limekazia kwa namna ya pekee umuhimu wa kukuza na kudumisha uhuru na demokrasia, kwa kujikita katika kuendeleza haki msingi, utu na heshima ya binadamu.

Kardinali Parolin, yuko mjini Prague kuanzia tarehe 13 Novemba 2014 ili kushiriki katika maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 25 tangu Agnese Bohemia alipotangazwa kuwa Mtakatifu kunako tarehe 12 Novemba 1989, tukio ambalo pia ni sehemu ya kumbu kumbu ya miaka 25 ya Mapinduzi ya kisiasa yaliyokomesha utawala wa Kikomunisti nchini humo.

Viongozi hawa wawili wamezungumzia kuhusu hija tatu za kichungaji zilizofanywa na Mtakatifu Yohane Paulo II pamoja na Baba Mtakatifu Benedikto XVI kunako mwaka 2009 pamoja na kuonesha matumaini kuwa, panapo majaliwa, Baba Mtakatifu Francisko anaweza pia kutembelea nchini humo, ili kujionea utajiri mkubwa wa maisha ya watu kiroho na kitamaduni. Baba Mtakatifu Francisko atakuwa na furaha, ikiwa kama Rais Zeman atamtembelea mjini Vatican panapo majaliwa.

Kardinali Parolin, akiwa nchini humo amepata fursa ya kuzungumza na viongozi wakuu kwa kuonesha mchango wa Kanisa katika ustawi na maendeleo ya wananchi, changamoto kwa sasa ni kukuza na kudumisha misingi ya uhuru na demokrasia ya kweli. Hii ni nchi ya Watakatifu Cyril na Metodi; nchi yenye utajiri wa tunu msingi za maisha ya kimaadili, kiroho na kitamaduni. Kanisa litaendelea kushikamana na wananchi wote kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi, lakini zaidi kwa kuonesha mshikamano na maskini pamoja na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, kwa kuwekeza katika sekta ya elimu, afya na maendeleo endelevu.

Kardinali Parolin amekutana na kuzungumza pia na wanadiplomasia wanaofanya kazi zao nchini Czech pamoja na kuwakumbuka Wakristo wengi waliojisadaka maisha yao kwa ajili ya kupandikiza mbegu ya Ukristo na leo hii Ukristo umeota mizizi na kukomaa licha ya madhulumu na nyanyaso zilizofanywa wakati wa utawala wa Kikomunisti dhidi ya Kanisa. Kardinali Frantisek Tomasek, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Prague, atakumbukwa na wengi kutokana na kusimama kidete kulinda na kutetea imani kwa Kristo na Kanisa lake.

Baada ya kuanguka kwa Ukomunisti, Czech ilianzisha uhusiano wa Kidiplomasia na Vatican, leo hii Kanisa linasonga mbele katika mchakato wa kuwahudumia wananchi wa Czech, kwa kukazia utu na heshima ya binadamu, haki, amani na upatanisho wa kitaifa.







All the contents on this site are copyrighted ©.