2014-11-14 14:02:16

Wizara ya afya, shirikianeni na sekta binafsi katika kutoa huduma bora kwa Watanzania!


Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda ameitaka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii nchini Tanzania ipanue wigo wa utoaji huduma za msingi kwa kuishirikisha zaidi sekta binafsi nchini. “Ninawasihi Waziri wa Afya na Naibu wake kwa vile ni wapya bado wabadili mtizamo wa wizara hii kwa kushirikisha zaidi wadau wa sekta binafsi kwenye utoaji wa huduma ili wasaidie kupunguza mzigo mkubwa ilionao Serikali,” alisema.
Ametoa kauli hiyo Ijumaa, Novemba 14, 2014 wakati akifungua Mkutano wa wa Kwanza wa Kitaifa wa Sekta ya Afya wa mwaka 2014 ulioanza Ijumaa kwenye ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Mwalimu Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu ambaye amefungua mkutano huo kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete aliyeko nje ya nchi kwa matibabu alisema: “Kuna tatizo la kukumbatia utoaji wa huduma ... tunazo hospitali kubwa za wilaya zinazomilikiwa na taasisi za dini. Hivi ni kwa nini kama Wizara msiwasaidie kuwahudumia watumishi wao au kuwapa ruzuku kwenye dawa ili kuwawezesha kutoa huduma kwa ufanisi zaidi?,” alihoji Waziri Mkuu na kushangiliwa na washiriki wa mkutano huo.
“Hata ukiangalia takwimu kwenye utoaji wa huduma za afya kupitia mifumo ya bima ya afya utabaini kuwa ni asilimia 18 tu wananchi wanatumia bima ya afya na kati ya hao, asilimia 15.3 ni mifuko ambayo imeanzishwa na Serikali. Ni kwa nini basi msiwasaidie wadau wa sekta binafsi ili wachangie huduma hii na idadi wa watumiaji wa mfumo huu iongezeke haraka?,” alihoji.
Akizumgumzia kuhusu uwiano kati ya daktari na mgonjwa, Waziri Mkuu alisema uwiano uliopo ni mbaya na kwamba hakuna njia ya haraka ya kupunguza tatizo hilo isipokuwa kwa kuishirikisha sekta binafsi kwenye ujenzi wa vyuo vikuu vya elimu ya tiba na sayansi za jamii.
“Uwiano wa sasa hapa nchini ni daktari mmoja kwa wagonjwa 75,000 wakati viwango vya kimataifa vinataka daktari mmoja awahudumie wagonjwa 7,000. Kwa wauguzi, hapa nchini muuguzi mmoja anahudumia wagonjwa 6,000 wakati viwango vya kimataifa vinataka muuguzi mmoja ahudumie wagonjwa 500,” alisema.
“Kwa uwioano huu safari bado ni ndefu. Tunapaswa tuangalie tutafanyaje ili watu binafsi waje kuwekeza kwenye elimu ya juu ya sayansi na tiba, wajenge vyuo vya tiba, wajenge hospitali kubwa, na sisi pia kwa upande wa Serikali ni lazima tuseme tunawapa vivutio gani hawa wawekezaji hadi wakubali kuwekeza kwenye eneo hilo,” alisema.
“Tunataka mkutano huo uje na mapendekezo ambayo mnataka Serikali iyafanyie kazi na hatimaye isaidie kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi,” alisema Waziri Mkuu.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufungua mkutano huo, Waziri Mkuu alisema Serikali inaendelea kudhibiti ugonjwa wa ebola kwenye vituo vya mipakani na kwenye viwanja wa ndege.
“Mpaka sasa hatujapata kesi ya ugonjwa wa Ebola hapa nchini... changamoto kubwa ni ukubwa wa mipaka yetu. Si wageni wote wanaoingia nchini wanapita kwenye vituo rasmi, wapo wanaotumia njia za vichochoroni. Rai yangu ni kuwaomba Watanzania wawe waangalifu kutambua ni wageni gani wanaingia kwenye maeneo wanayoishi,” alisema.
Mkutano huo wa siku mbili unamalizika Jumamosi, Novemba 15, 2014.








All the contents on this site are copyrighted ©.