Rais Tasso wa Perù akutana na kuzungumza na Papa Francisko mjini Vatican
Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 14 Novemba 2014 amekutana na kuzungumza na
Rais Ollanta Moises Humala Tasso wa Perù na ujumbe wake waliomtembelea mjini Vatican.
Baadaye, Rais Tasso amekutana na kuzungumza na Askofu mkuu Dominique Mamberti, aliyekuwa
Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican, bila
uwepo wa Kardinali Pietro Parolin ambaye kwa sasa yuko nje ya Vatican kikazi.
Viongozi
hawa wawili wamesifu mahusiano mema kati ya Vatican na Perù na kwa namna ya pekee
kabisa, kuhusiana na mchango wa Wakristo katika mchakato wa majiundo ya wananchi wa
Perù bila kusahau mchango wa Kanisa katika ustawi na maendeleo ya wengi nchini humo
katika kukuza na kudumisha utu na heshima ya binadamu; katika masuala ya kitamaduni
na maendeleo ya watu.
Baba Mtakatifu na mgeni wake walibadilishana mawazo kuhusiana
na masuala ya kisiasa na kijamii yanayojiri katika Kanda hii, kwa kujikita zaidi katika
vichocheo vya maendeleo ya mtu mzima sanjari na utunzaji bora wa mazingira.