Jubilee ya miaka 25 tangu Agnese wa Bohemia alipotangazwa kuwa Mtakatifu
Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kuanzia tarehe 13 hadi tarehe 16
Novemba 2014 anafanya hija ya kichungaji nchini Prague, kama sehemu ya maadhimisho
ya Jubilee ya miaka 25 tangu Agnese wa Bohemia, alipotangazwa na Papa Yohane Paulo
II kuwa Mtakatifu, tukio lililofanyika tarehe 12 Novemba 1989.
Tarehe 16 Novemba,
wananchi wa Prague wanakumbuka siku ambayo siasa za Kikomunisti zilipobwagwa chini
na nchi ikaanza mchakato wa demokrasia. Akiwa nchini humo, Kardinali Parolin anakutana
na viongozi mbali mbali. Kilele cha ziara yake ya kikazi ni Jumamosi, tarehe 15 Novemba
2014, kwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, kwa heshima ya Mtakatifu Agnese, Ibada
itakayofanyika kwenye Kanisa kuu Mtakatifu Vito.
Katika Ibada hii, Kardinali
Parolin atabainisha tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu zilizompelekea kujisadaka
kwa ajili ya maskini na wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii ya wakati
wake. NI Mama aliyekuwa na huruma na upendo wa pekee kwa wagonjwa, ndiyo maana Kardinali
Parolin atakutana na Maaskofu wa Parague Hospitalini hapo. Jumapili tarehe 16 Novemba,
2014, Kardinali Pietro Parolin ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu katika Parokia
ya Mtakatifu Agnese.