2014-11-14 08:33:28

Dumisheni majadiliano ya kidini na waamini wa dini ya Kiislam ili kudumisha amani!


Askofu Benjamin Ndiaye, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu kutoka Afrika Magharibi, linalozijumuisha nchi za Senegal, Mauritania, Cape Verde na Guinea Bissau, anasema, binadamu anaishi katika ulimwengu unaobadilika kwa kasi kubwa mno, mwaliko kwa watu kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu, kwani watu kwa sasa wanategemeana kwa hali na mali.

Kuibuka kwa Kikundi cha Jihadi huko Mashariki ya Kati ni jambo linalotishia amani, ustawi na usalama wa watu na mali zao; ni tishio katika amani na uhuru wa kuabudu, ambao ni haki msingi kwa kila binadamu. Watu wanapaswa kutambua kwamba, leo hii ni vigumu kuishi peke peke kama kisiwa, mambo yamebadilika kutokana na utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Kwa miaka mingi waamini wa dini ya Kiislam na Kikristo waliishi kwa amani na utulivu, kwa mfano nchini Senegal. Hii ni kutokana na busara na hekima inayojikita katika Mapokeo ya watu.

Ili kulinda, kujenga na kudumisha misingi ya haki na amani, kuna haja kwa waamini wa dini mbali mbali kuheshimiana, kuthaminiana na kusaidiana kama ndugu; kila upande ukijitahidi kujenga mazingira bora zaidi yatakayosaidia kukuza na kudumisha uhuru wa kuabudu. Maaskofu Katoliki kutoka Senegal, Mauritania, Cape Verde na Guinea Bissau, walipokutana hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican wakati wa hija yao ya kitume, alikazia umuhimu wa kudumisha majadiliano ya kidini miongoni mwa Wakristo na Waislam, ili kweli amani iweze kupatikana kati ya watu!

Majadiliano ya kidini kati ya waamini wa dini hizi mbili ni jambo linalowezekana, lakini lazima livaliwe njuga ili kuweza kutekeleza dhamana hii nyeti katika ustawi na maendeleo ya wananchi wengi.







All the contents on this site are copyrighted ©.