2014-11-14 08:07:51

Chakarika mwanangu hadi kieleweke!


Mpishi akitataka kupika ugali inambidi apime unga kama unalingana na wingi wa maji aliyoandaa. Asipofanya hivyo, maji yakiwa machache, ataishia kukaanga unga au itambidi kuongeza maji baridi na ugali utakuwa mbichi. Maji yakiwa mengi kuzidi unga ataishia kukoroga uji badala ya ugali. Mlaji wa ugali ndiye mwamuzi kwamba mpishi amefaulu kupima sawasawa “unga na maji” pale anapofurahia chakula na kumsifu mpishi.

Waswahili wanasema “Pima unga na maji” ili kumtahadharisha mtu atumie busara ya kupima jambo kabla ya kulichagua. Katika Injili ya dominika tatu mfululizo tunaletewa wahusika waliofaulu na wale walioshindwa “kupima unga na maji” katika maamuzi ya matendo yao, hatimaye wengine wakafanikiwa kupika ugali uliomfurahisha mlaji, na wangine wakaishia kukoroga na kujikoroga au kukaanga na kujikaanga wenyewe.

Dominika iliyopita tulipelekwa kwenye mnuso wa arusi tulikowaona wanapambe kumi. Wapambe wapumbavu “nuksi” walishindwa kupima unga na maji wakaishia “kulikoroga” na “kujikoroga” wenyewe, pindi wale wenye busara wakaingia katika furaha ya mnuso wa arusi ya Bwana. Kadhalika Injili ya leo na ya dominika ijayo zinatualika kupima “unga na maji” katika maamuzi yetu na jinsi tunavyocheza na kete ya uhai wa maisha yetu.

Leo tutawaangalia wajasiriamali wanavyopima unga na maji katika miradi yao. Kabla ya kuona fundisho analotaka kulitoa Yesu kwa wajasiria mali, budi tuelewe kwanza maana ya neno hilo ujasiriamali. Neno Ujasiriamali lina asili ya Kifaransa " Entreprendre" sawa na kutekeleza au kufanya shughuli fulani mwenyewe, yaani kujiajiri. Mjasiriamali ni mtu mwenye hamasa kubwa ya kuleta mabadiliko chanya katika hali yake ya kiuchumi. Mjasiriamali anajiajiri mwenyewe katika sekta anayoipenda, mathalani katika kilimo, ufugaji au biashara. Mjasiriamali ni mtu anayejitosa, na yuko utayari kukabili hatari zozote zinazoweza kujitokeza katika biashara au mradi wake.

Mfano wa Injili ya leo unahusu kupima unga na maji katika suala la matumizi ya mtaji waliowezeshwa wajasiriamali. Kama mjasiriamali ni mkulima, basi tungeweza kusema amepewa mbegu ya kupanda, au kama ni mfugaji huyo kapewa dume la mbegu. Katika mfano huu kuna hatua tatu: hatua ya kwanza tunakutana na mtu mmoja aliyekuwa tayari kuwawezesha watumishi wake. Akawagawia mtaji wa kujiendeleza katika maisha yao kabla hajaondoka kwenda safari refu.

Hatua ya pili, ni kile kipindi alichonacho mjasiriamali ili afanyie kazi mtaji aliopata. Hatua ya tatu ni ile ambayo mtoa mtaji anarudi na kuangalia jinsi watumishi hawa walivyotumia mtaji waliopewa, kama wamezalisha, au wamekula mtaji.

Wahusika wa mfano huu ni rahisi sana kuwaelewa. Mhusika wa kwanza anayetoa mtaji na kusafiri ni Bwana Yesu mwenyewe. Huyo kwa kupaa mbinguni anaonekana kama ametoweka machoni petu, lakini kabla ya kuondoka anatupatia mtaji, yaani anatuwezesha. Anampatia kila mmoja wetu uwezekano wa kuishi Habari njema aliyoitangaza. Kisha anaondoka lakini atarudi tena. “Kristu alikufa, Kristu alifufuka, Kristu atakuja tena.”

Mhusika wa pili ni watumishi. Hawa ndiyo wajasiriamali, walioamua kufuata sera za maisha ya Kristu. Wajasiriamali hao ni sisi wote hasa wakristu. Wajasiriamali hao wanaoitwa watumishi siyo wafanyakazi wa mshahara, bali wamejizatiti kufuata sera za Bwana Yesu, yaani ni wale waliotaka kuwezeshwa ili wafanye mradi na hatimaye kukwamua maisha yao. Ni wale walioamua kuishi ukristu, yaani kumwenzi Kristu na ufalme wa Baba yake.

Mtumishi wa Bwana ni yule aliyetoa maisha yake katika mradi wa Mungu. “Mimi ni mtumishi wa Bwana nitendewe ulivyonena”. Mtaji au talenti inayosemwa hapa siyo kitu kingine isipokuwa imani ya Kristu. Imani ambayo Mungu ametupatia kwa njia ya Mwanae Kristu inabidi kuifanyia kazi. Ni dhahiri pia kwamba imani hiyo anayotoa Mungu hutegemea na uwezo (sifa) wa mtu.

Mtaji huo wa imani ni wa kufuata sera za Ufalme wa Mungu ambao Bwana Yesu ameuingiza kwa mahubiri yake, na kwa huduma zake mbalimbali hivi akaubadili ulimwengu “Ametuma Roho wake na vitu vyote vikawa vimeumbwa upya”. Mtaji wa imani waliopewa watumishi hawa ni ule uwezo wa kutoa pepo, wa kutofanya vita, kusaidia wengine, wa kupenda, kudumisha haki nk. Wajasiriamali wote waliopewa mtaji wa imani kwa Kristu, wanaalikwa kutumia nguvu zao zote kuleta matunda yanayoonekana katika mtaji huo waliokabidhiwa.

Mtumishi wa kwanza amepata mtaji wa talanta tano, namba hiyo inataka kuonesha wingi au ukubwa. Mtumishi aliyepokea talenti hiyo kubwa, anaithamini na bila kupoteza muda anaanza kuifanyia kazi mara moja. Ndivyo ilivyo paji la imani kwa Kristu ni talanta kubwa sana, yabidi kuifanyia kazi mara moja. Kadhalika yule aliyepata talenti mbili anaithamini na kuifanyia kazi mara moja. Lakini mtumishi wa tatu, anapima kwanza unga na maji anaamua kutoitendea kazi badala yake anaichimbia ardhini.

Sehemu ya tatu, inahusu kupima jinsi kila mmoja wa wahusika wa watumishi alivyowajibika na kuchakalika. Bwana anarudi na kuangalia jinsi kila mjasiriamali alivyoifanyia kazi ule mtaji aliopewa. Mjasiriamali wa kwanza anaonesha mtaji na faida juu. Bwana anamwagia sifa kedekede na kumwambia “vyema mtumishi mwema na mwaminifu”. Ndizo sifa mbili anazopewa mtumishi huyu.

Yaani ni mwema na mwaminifu, kwa sababu ameyatoa maisha yake katika kuishi imani yake kwa Mungu. “Nimemwezesha mtu huyu kwa kumpa mtaji ambao umeweza kutoa matunda.” Kisha anapewa nishani ambayo ni kushiriki katika furaha ya kazi aliyofanya, anaambiwa “Ingia katika furaha ya Bwana”, yaani mtumishi huyu sasa anakuwa sehemu ya ubinadamu ulioingia katika historia ya ufalme wa Mungu ulioujengwa na Kristu katika ulimwengu huu. Hiyo ndiyo maana ya kuingia katika furaha ya Bwana.

Mtumishi wa tatu akapima unga na maji, yaani uwezo alio nao, na mtaji aliopewa pamoja na ukali wa Bwana aliyetoa mtaji, akaona asijaribu hata kupika ugali, atashindwa tu, hivi akasema: “Nalitambua ya kuwa wewe u mtu mgumu, wavuna usipopanda, wakusanya usipotawanya; nikaogopa, nikaenda nikaificha talanta yako katika ardhi; tazama, unazo iliyo yako.” Mtumishi huyu aliyewezeshwa kwa kupewa mtaji wa imani hakuifanyia kazi. Hoja nzito ya mtumishi huyu, ameieleza yeye mwenyewe kwamba “Mimi nilikuogopa, kwa hiyo ninakurudishia mtaji wako na tuishiane”.

Kitendo alichoonesha mjasiriamali huyu chaonekana kuwa kama cha busara, kumbe, huo ulikuwa ni woga. Nadhani woga wa mtumishi huyu unatokana na kumwona yule Bwana kuwa kama nyapara na mtawala mkali, anayekuhukumu, anayeadhibu. Hakuutumia mtaji ule kwa kuogopa kukosea. Bwana huyu naye hamwonyi mtumishi huyu kwamba asingetakiwa kumfikiria hivyo, bali anazidi kumkandamiza na kumwambia: “Kama uliniogopa kweli walau ungetumia busara ya kuwekeza kwa watoa faida.” Kama mtaji huo ungekuwa ni upendo, basi mjasiriamali huyu wa upendo ameogopa kupenda.

Woga wa mtumishi huyu, unatuwakilisha sisi tunaomwogopa Mungu na tulio na woga unaotutia ganzi ya kutoweza kuwajibika na kujihusisha katika kazi ya upendo. Adhabu ya mtu asiyeendeleza mtaji aliopata wa Bwana ni kukosa kuingia katika furaha ya Bwana wake. Hiyo siyo hukumu ya kwenda motoni, bali ni kutoshiriki katika ufalme wa Mungu tulionao sasa hapa ulimwenguni.

Katika ujasiriamali wa mtaji wa imani kwa Mungu tuliyopewa na Kristu, tunamkuta yule asiyejisikia kuwajibika na yule aiyekuwa shujaa wa kuzalisha jema la Bwana. Tunaalikwa sote kutendea kazi mtaji wa imani na upendo tuliopewa au hata kuweka benki yaani kujikabidhi kwa jumuia wanaoweza kuonesha upendo huo.

Hatima ya mfano huu ni hii: “Kwa maana kila mwenye kitu atapewa, na kuongezewa tele, lakini asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang’anywa.” Ukweli ni kwamba mjasiriamali yeyote anayejishughulisha atafanikiwa na kuwa tajiri. Kadhalika utajiri wa ufalme wa Mungu ukijishughulisha, unaongezeka. Mathalani zile jumuia za kikristu zenye ukarimu, utaziona zinavyoendelea kuwa hai, pindi zile zinazojirudi na kujifikiria zenyewe tu, hizo huzeeka, hudumaa na hakuna atakayeshanga zinapofifia na kufa zenyewe tu.

Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.