2014-11-13 08:38:47

Watanzania nchini Italia kukutana na Makamu wa Rais Bilal, hapo tarehe 18 Novemba, 2014


Dr. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anatarajiwa kukutana na kuzungumza na Watanzania wanaoishi nchini Italia hapo tarehe 18 Novemba 2014 katika Ukumbi wa mikutano wa Hotel Ambasciatori Palace, iliyoko mtaa wa Vittorio Veneto namba 62, mjini Roma.

Taarifa rasmi iliyotolewa na Ubalozi wa Tanzania nchini Italia inaonesha kwamba, mkutano huu kati ya Makamu wa Rais na Watanzania wanaoishi nchini Italia unatarajiwa kuanza hapo saa 9: 00 Alasiri. Watanzania wanahamasishwa kuhudhuria mkutano huu, ili kuweza kuzungumza na Makamu wa Rais kuhusu masuala mbali mbali kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, hasa wakati huu, Tanzania inapojiandaa kupiga kura ya maoni kuhusu Katiba Mpya na Uchaguzi mkuu 2015.

Taarifa ya ubalozi wa Tanzania nchini Italia inaonesha inasema kwamba, unaendelea kupokea maombi ya pasipoti hususan zile zinazomaliza muda wake mwaka 2015. Pamoja na Afisa wa Ubalozi pia kutakuwa na Maofisa wakuu wawili wa uhamiaji kutoka Makao makuu Dar es Salaam na Zanzibar kwa ajili ya kupokea maombi ya pasipoti.

Kwa watanzania wanaoishi nje ya mji wa Roma wamepangiwa tarehe 15 hadi tarehe 16 Novemba 2014 kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 12 jioni na shughuli hii itafanyika mjini Napoli. Kwa watanzania wanaoishi nchini Ugiriki, wao watashughulikiwa mjini Athens, hapo tarehe 18 hadi tarehe 20 Novemba 2014 kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni mjini Istanbul. Kuanzia tarehe 24 - 25 Novemba 2014, itakuwa ni fursa kwa watanzania wanaoishi Kaskazini mwa Italia, wao watahudumiwa mjini Modena kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni.







All the contents on this site are copyrighted ©.