Vita inaharibu, inaua na kuwatumbukiza watu katika umaskini!
Kanisa linaichangamotisha Jumuiya ya Kimataifa kuangalia dhana ya vita katika mwelekeo
mpya, ili kudumisha misingi ya haki, amani, ustawi na maendeleo ya binadamu. Vita
ni balaa na njia isiyofaa kwa kutatua na kumalizamatatizo yanayozuka kati ya mataifa.
Vita inatabia ya kuzua migogoro na kinzani mpya na zenye utata zaidi. Vita inapozuka
husababisha mauaji ya kinyama yasiyo ya lazima na kwamba, ni tukio ambalo linahatarisha
hali ya maisha ya binadamu kwa sasa na kwa siku za usoni.
Mababa wa Kanisa
wanafundisha kwamba, hakuna kinachoweza kupotea kwa kuwa na amani, lakini kinyume
chake ni kwamba kila kitu kinaweza kupotea kwa vita. Madhara ya mapambano ya silaha
yanamgusa mtu mzima: kiroho na kimwili na kwamba, vita ni kushindwa kwa utu wa kweli
wa binadamu wote. Vita daima ni kushindwa kwa binadamu.
Baba Mtakatifu Francisko
katika ujumbe wake kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii anasema kwamba, vita inasababisha
uharibifu mkubwa, inaangamiza, inawadumbukiza watu katika dimbwi la umaskini, njaa
na magonjwa. Baba Mtakatifu anamwomba Yesu Kristo, Bwana wa amani, awajalie walimwengu
zawadi ya amani.