2014-11-13 07:28:59

Ukatili na unyama unaojificha kwenye biashara haramu ya dawa za kulevya!


Baba Mtakatifu Francisko, mwishoni wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 12 Novemba 2014 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, aliwakumbuka kwa namna ya pekee Wakristo wanaoteswa na kunyanyaswa sehemu mbali mbali za dunia pamoja na wanafunzi 43 kutoka Mexico waliotekwa nyara na hatimaye kuuwawa kikatili. Taarifa iliyotolewa na Mwanasheria mkuu wa Serikali Bwana Jesus Murillo inasema kwamba, wanafunzi hao waliuwa na hatimaye kuchomwa moto ili kufuta ushahidi.

Hadi sasa Meya wa mji wa Iguala pamoja na mke wake wametiwa nguvuni ili kujibu tuhuma zinazowakabili za kuteka na hatimaye kuamuru wanafunzi hao kuuwawa kinyama, hali ambayo hadi sasa imesababisha machafuko ya kijamii nchini Mexico, kwani watu wanataka kufahamu ukweli wa tukio hili la kinyama. Baba Mtakatifu anasema tukio hili linaonesha ukatili mkubwa unaojificha kwenye biashara haramu ya dawa za kulevya. Baba Mtakatifu amewahakikishia wote walioguswa na tukio hili la kikatili uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala.

Baba Mtakatifu amekumbuka pia mkataba wa amani kati ya Argentina na Chile. uliotiwa sahihi miaka thelathini iliyopita, wakati alipokuwa anasalimia kikundi cha wanajeshi kutoka Chile, amewataka viongozi wa kisiasa kudumisha mchakato wa majadiliano, ili kujenga na kudumisha haki na amani kati ya nchi jirani na kwamba, hakuna sababu ya msingi kwa nchi jirani "kutunishiana misuli". Pale watu wanapoonesha utashi wa majadiliano katika haki na ukweli, hapo kuna uwezekano wa kupatikana kwa suluhu.

Baba Mtakatifu Francisko amemkumbuka kwa namna ya pekee Mtakatifu Yohane Paulo II pamoja na Kardinali Samorè waliowezesha nchi hizi mbili kufikia muafaka na hatimaye, kuweka sahihi makubaliano ya amani. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, hata wale watu wanaoendelea kukabiliana na kinzani za aina mbali mbali, wanaweza kupata suluhu ya kudumu kwa njia ya majadiliano yanayojikita katika ukweli na uwazi badala ya kukimbilia kwenye ukatili unaojificha katika vita.

Baba Mtakatifu anawataka viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kujenga dhamiri nyofu ili kusaidia hatima ya Wakristo wanaoendelea kuteseka kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Wananchi wana haki ya kupata amani, usalama na utulivu katika nchi zao wenyewe wakati wanapotumia haki yao ya kuabudu, changamoto kwa waamini kuendelea kuwa imara na thabiti katika imani yao, licha ya madhulumu na nyanyaso wanazoweza kukabiliana nazo.

Kwa sasa kuna idadi kubwa ya Wakristo wanaolazimika kuzikimbia nchi zao kutokana na nyanyaso na dhuluma za kidini, kiasi kwamba, kwa sasa wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha. Serikali ya Yordan inaendelea kupokea idadi kubwa ya wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi ya maisha yao, kwani hii ndiyo nchi pekee huko Mashariki ya Kati ambayo amani bado inatawala kati ya Serikali na wananchi wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.