Lifuatalo ni tamko la Waziri waAafya na Ustawi wa Jamii Mhe. Dkt. Seif Suleiman Rashid
[MB]) kuhusu Siku ya Kisukari Duniani, tarehe 14 Novemba 2014.
Ndugu Wananchi, Siku
ya kisukari Duniani, huadhimishwa duniani kote kila mwaka ifikapo tarehe 14 ya Mwezi
Novemba. Siku ya kisukari Duniani ilianzishwa mwaka 1991 na mashirika mawili ya kimataifa
ya International Diabetes Federation [IDF] na World Health Organization [WHO] baada
ya kuona Ugonjwa wa kisukari unaongezeka sana duniani kote. Ilipendekezwa tarehe 14
ya mwezi Novemba kila mwaka kwa sababu ndio siku ya Mwanasayansi maarufu Sir Frederic
Banting alipozaliwa na ndiye mgunduzi wa dawa ya Insulin na alikuwa wa kwanza kuitumia
kwa wagonjwa wa Kisukari.
Tanzania kama zilivyo nchi nyingine duniani inaadhimisha
siku hii, kwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kushirikiana na Chama cha Ugonjwa
wa Kisukari Tanzania kutoa elimu ya umuhimu wa kuzuia na kujikinga na madhara mbalimbali
yatokanayo na ugonjwa wa kisukari.
Ndugu Wananchi, Ugonjwa wa Kisukari
ni hali ambayo hutokea wakati sukari katika damu inapokuwa nyingi kupita kiwango cha
kawaida kwa muda mrefu. Sukari hutumiwa na mwili ili kupata nishati lishe. Ili mwili
uweze kutumia sukari inayotokana na vyakula, unahitaji kichocheo cha insulin. Insulin
husaidia sukari kuingia kwenye chembechembe hai ili kutengeneza nishati lishe. Ugonjwa
wa kisukari unasababishwa na kichocheo hiki kupungua au kutofanya kazi kama inavyotakiwa,
hivyo kiwango cha kisukari kinabaki kikubwa kwenye damu kwa sababu sukari haikuwezeshwa
kuingia kwenye chembechembe hai za mwili.
Mara nyingi, watu wengi hawajitambui
ya kuwa wana ugonjwa huu. Wengine wanakuwa na dalili lakini hawachukui hatua mapema.
Dalili za kisukari ni rahisi kuzitambua nazo ni: kiu isiyoisha, kukojoa mara kwa mara,
kupungua uzito, kusikia njaa kila wakati na mwili kukosa nguvu. Ukiwa na dalili hizi
nenda hospitali ukapime sukari.
Ndugu Wananchi, Tafiti za ugonjwa wa kisukari
zinaonyesha kuwa mwaka 2007 kulikuwa na wagonjwa 246 milioni duniani. Takwimu za mwaka
2012 zinaonyesha kuwa kulikuwa na wagonjwa 371 milioni ulimwenguni kote, Takwimu za
mwaka 2013, zinaonyesha kuwa kulikuwa na wagonjwa 382 duniani kote.Ifikapo mwaka 2035
kutakuwa na wagonjwa 592 millioni. Katika bara la Afrika kulikuwa na wagonjwa wa kisukari
19.8 millioni mwaka 2013 na wataongezeka mpaka million 41.4 ifikapo mwaka 2035, ambapo
nusu ya wagonjwa hawa walikuwa hawajaanza matibabu. Asilimia 80 ya wagonjwa wote wa
kisukari ulimwenguni wanaishi katika nchi zinazoendelea, ikiwemo Tanzania.
Utafiti
uliofanyika mwaka 2012 na kuhusisha wilaya 50 nchini Tanzania ulionyesha ya kuwa asilimia
9.1 ya Watanzania wenye umri wa miaka 25 na kuendelea wana ugonjwa wa kisukari. Katika
nchi 10 zinazoongoza kwa kisukari Barani Afrika Tanzania inashika nafasi ya 8.
Ndugu
Wananchi, Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Siku ya kisukari Duniani mwaka 2014 ni “Ulaji
unaofaa, huanza na mlo wa asubuhi” Kauli mbiu hii inalenga kuelimisha na kuhamasisha
jamii juu ya ulaji unaofaa ili kuepuka matatizo mbalimbali yanayotokana na ugonjwa
wa kisukari katika jamii, Pamoja na magonjwa mengine yasiyo ya kuambukiza yanayoendana
na kisukari ni pamoja na magonjwa ya moyo na mishipa ya damu, saratani na magonjwa
sugu ya njia ya hewa.
Ulaji unaofaa ni pamoja na kula chakula mchanganyiko
cha kukutosha kukua na kuwa na uzito wa kawaida na chenye virutubisho vyote vinavyohitajika
mwilini. Kwa mfano vyakula vya wanga vinasaidia kuupa mwili nguvu na joto, protein
husaidia kujenga mwili na kutengeneza vichocheo mbalimbali, vitamin na madini hulinda
mwili dhidi ya magonjwa. Mambo yanayoongeza uwezekano wa kupata magonjwa haya yasiyo
ya kuambukiza ni pamoja na ulaji usiofaa hasa matumizi ya chumvi kwa wingi, mafuta
na sukari, uzito uliozidi, unene uliokithiri, kutofanya mazoezi, uvutaji wa sigara
na bidhaa zitokanazo na tumbaku, unywaji pombe kupita kiasi na msongo wa mawazo.
Ndugu
Wananchi, Ulaji usiofaa ni kula chakula bila kuzingatia aina na kiasi kulingana
na mahitaji ya mwili. Hii huweza kusababisha kupungua au kuzidi kwa virutubishi mwilini.
Ulaji usiofaa ni pamoja na kula vyakula vyenye mafuta mengi hasa yale yatokanayo na
wanyama, kula vyakula vyenye chumvi nyingi, sukari nyingi, kula chakula kupita kiasi,
kukoboa nafaka na kutokula mbogamboga na matunda kiasi cha kutosha.
Kutofanya
Mazoezi ya mwili chakula kinacholiwa kwa kawaida hutumika na mwili kufanya kazi mbalimbali.
Iwapo chakula hakitatumika hubadilishwa na kuhifadhiwa mwilini kama mafuta na hatimaye
husababisha uzito kuzidi. Mambo yanayochangia mwili kutotumia chakula kilicholiwa
ni pamoja na kukaa muda mrefu bila kufanya mazoezi ya mwili, kwa mfano : kuketi ofisini,
darasani, kukaa na kuangalia runinga kwa muda mrefu, kutumia lifti kwenda ghorofani
badala ya ngazi, kupanda gari mahali pa umbali mfupi badala ya kutembea kwa miguu,
na kutoshiriki katika michezo.
Uzito na unene uliozidi uzito unakuwa umezidi
pale ambapo uzito wa mtu unakuwa asilimia 20 zaidi ya uzito unaotakiwa. Ili kupima
hali hiyo viashiria mbalimbali hutumika; njia inayotumika mara nyingi ni ile ya uwiano
wa uzito na urefu wa mwili kulingana na viwango maalumu vilivyowekwa.
Msongo
wa mawazo huweza kusababisha ulaji usiofaa na huweza kufanya mifumo mbalimbali ya
mwili kutofanya kazi vizuri.
Matumizi ya pombe huchangia katika kuongeza uzito
mara nyingi. Unywaji wa pombe za aina zote huendana na ulaji wa vyakula kwa wingi
ambayo huchangia kuongeza uzito. Pombe yenyewe ikizidi inaweza kuharibu maini, kusababisha
utapiamlo kwa wale wanaoishia kunywa pombe zaidi ya kula chakula.
Uvutaji
wa Sigara na matumizi ya bidhaa zitokanazo na Tumbaku licha ya kuwa ni matumizi yasiyo
na tija, tumbako husababisha madhara mengi mwilini yakiwemo magonjwa ya moyo na mishipa
ya damu, saratani na magonjwa sugu ya njia ya hewa.
Ndugu Wananchi, Ili
kuzuia ugonjwa wa kisukari na maradhi mengine yasiyo ya kuambukiza ni muhimu kufuata
kanuni za afya ambazo ni ulaji bora, na mtindo bora wa maisha ambao ukifuatwa vyema
huweza kwa kiasi kikubwa kuzuia mtu kupata kisukari au kwa mtu ambaye tayari ana ugonjwa
wa kisukari hupunguza uwezekano wa kupata madhara makubwa ya kiafya.
Ndugu
Wananchi, Serikali inaendelea na utekelezaji wa Sera ya Afya (2007) ambayo inalenga
kutoa huduma kwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza ikiwemo kisukari kwa kushirikiana na
wadau mbalimbali wa ndani ya nchi na wa kimataifa. Aidha, serikali, sekta binafsi,
mashirika ya kimataifa na taasisi zinazotoa huduma bila faida zinaendelea kuandaa
na kurekebisha sheria, kanuni na taratibu zinazoimarisha uzuiaji na udhibiti wa magonjwa
yasiyo ya kuambukiza.
Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inatumia
maadhimisho haya kuwa sehemu ya uhamasishaji kwa jamii kama ilivyo kwenye nchi zote
duniani.
Ndugu Wananchi, Serikali inaeendelea kuandaa miongozo na mikakati
ya kisera kwa kushirikisha jamii katika kudhibiti magonjwa yasiyo ya kuambukiza, ikiwemo
kisukari. Serikali imeimarisha ushiriki wa sekta mbalimbali za umma na za binafsi
katika kukabiliana na vyanzo vinavyosababisha magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
Ndugu
wananchi, Kwa kutambua gharama za kutibu ugonjwa wa kisukari, kuanzia mwaka 1993,
serikali ilitoa msamaha kwa wagonjwa wote wa kisukari kutochangia gharama za matibabu
na inajitahidi kwa uwezo wa bajeti yetu pamoja na wahisani wetu kuhakikisha kuwa dawa
muhimu zinapatikana. Kwa sasa watoto wote na vijana chini ya miaka ishirini na miwili
walio na kisukari wanapata mahitaji yao yote kupitia kliniki za kisukari zilizopo
nchini.
Kuanzia mwaka 2012, serikali pamoja na washirika wake inatekeleza mpango
wa kuthibiti ugonjwa wa kisukari nchini. Lengo ni kuwa na kliniki hizo hadi katika
hospitali za wilaya kwa sasa zipo kliniki za kisukari kwenye ngazi za mikoa na kuwapatia
wananchi elimu ya ugonjwa wa kisukari ili waweze kushiriki kikamilifu kwenye kinga
na tiba ya magonjwa haya.
Tanzania inaungana na mataifa yote duniani kutekeleza
azimio la Umoja wa Mataifa la mwaka 2011 la kuhakikisha ya kuwa kuna mpango kabambe
wa kuthibiti magonjwa yasiyo ya kuambukiza. Nchi yetu inaungana na mataifa mengine
kuhakikisha ya kuwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza yanapungua kwa asilimia 25 ifikapo
mwaka 2025. Sasa unaandaliwa mpango huo kwa kukishirikiana na wadau wengine wahusika.
Ndugu
wananchi, Kwa bahati mbaya, unaweza kuwa na ugonjwa huu kwa muda mrefu bila kuwa
na dalili nilizotaja hapo awali. Hata hivyo, jinsi sukari inavyokuwa juu, inaharibu
mishipa ya damu na ya fahamu, macho, figo na kusababisha upofu, moyo na figo kushindwa
kufanya kazi, na miguu kufa ganzi, kuwa na vidonda. Hivyo, ninatoa wito kwa kila
mmoja wetu kuhakikisha kuwa anapima afya yake kwa kuwa ugonjwa huu unaweza usionyeshe
dalili yoyote mapema. Ni vyema kila mmoja akapima afya yake mara kwa mara ili kutambua
hali yake ya afya. Endapo utatambuliwa kuwa una ugonjwa wa kisukari tumia huduma za
afya kulingana na ushauri utakaopewa na wataalam wa afya.
Kwa wale ambao wameshajitambua
kuwa na matatizo ya kisukari lakini hawatumii huduma za afya ipasavyo, nawaasa watumie
huduma za afya zilizopo kwa manufaa ya afya zao na kuepusha athari zinazotokana na
ugonjwa ya kisukari.