2014-11-13 09:26:21

Ufisadi wa fedha ya umma umesababisha njaa na umaskini mkubwa nchini Malawi!


Askofu Joseph Mukasa Zuza, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi, hivi karibuni wakati wa hija ya kitume inayofanywa na Maaskofu Katoliki mjini Vatican walau kila baada ya miaka mitano anasema, kuna wananchi wengi wa Malawi wanakufa kutokana na huduma mbaya za afya pamoja na ukosefu wa dawa msingi. Haya ndiyo matokeo ya kashfa ya ufisadi uliofanywa na baadhi ya viongozi wa Serikali na kisiasa, kiasi cha kusababisha kashfa, iliyopelekea wafadhili mbali mbali kusita kuchangia bajeti ya Serikali ya Malawi.

Jumuiya ya Ulaya ilikuwa inachangia kiasi cha asilimi 40% ya Bajeti yote ya Malawi, lakini kwa sasa Jumuiya hii pamoja na wafadhili wengine wamesitisha kuchangia bajeti ya Serikali ya Malawi, hadi pale watakapokuwa na uhakika wa matumizi bora ya fedha ya umma. Sekta ya afya ni kati ya maeneo ambayo yameathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na ufinyu wa bajeti ya Serikali, kiasi kwamba watu wanafariki dunia na hawana tena matumaini.

Kanisa limekuwa ni mdau mkubwa katika sekta ya afya, lakini kwa bahati mbaya kwa miaka mingi limeendelea kutegemea misaada kutoka nje ya nchi na hali kwa sasa ni mbaya, changamoto kwa waamini kujifunga mkanda ili kulitegemeza Kanisa mahalia. Kutokana na ukosefu wa bajeti, wananchi wengi wa Malawi watakabiliwa pia na uhaba mkubwa wachakula kutokana na mavuno ya mwaka huu kuwa hafifu. Hali hii itaongeza kwa kiasi kikubwa kiwango cha umaskini nchini Malawi, lakini zaidi kwa wale wanaoishi vijijini.

Vyombo vya sheria vinasema kwamba, kiasi cha dolla millioni 30 ziliibwa kutoka Serikalini. Takwimu zinaonesha kwamba, tangu Mwaka 2013 watu 70 wametiwa mbaroni kutokana na ufisadi na wizi wa mali ya umma.







All the contents on this site are copyrighted ©.